TFF kupanga mechi ya uzinduzi wa uwanja

Uwanja mkuu wa Taifa ambao ulikuwa katika matengenezo kwa takribani miezi mitatu, unatarajiwa kufunguliwa rasmi kuanzia Novemba 24 mwaka huu.



Akizungumza leo wakati wa kukagua uwanja huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema Uwanja umekamilika na hauna tena vipara vilivyokuwa vinaonekana awali.

Dkt. Mwakyembe amesema, serikali itakabidhiwa uwanja huo rasmi na Kampuni ya Sport Pesa ndani ya siku 10 zijazo, ambapo ameiomba TFF kwa kushirikiana na bodi ya Ligi kupanga mechi moja ichezwe katika zoezi la uzinduzi.

“Uwanja umekamilika na leo nimeukagua na kuridhishwa na ukarabati mkubwa uliofanywa, wameniambia baada ya siku 10 utakuwa tayari hivyo nimewaomba TFF kuangalia uwezekano wa kutafuta japo mechi moja ichezwe wakati wa ufunguzi Novemba 24,” amesema Mwakyembe.



Aliongeza kuwa wapo vijana sita ambao wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa uwanja hivyo ameomba kuangaliwa kwa ajira zao ili waweze kutumika katika viwanja vingine vya mikoani.

Aidha waziri Mwakyembe amewataka mashabiki na Watanzania kwa ujumla kushirikiana katika kuutunza uwanja huo kwani hadi sasa marekebisho yamechukua gharama kubwa ambazo ni zaidi ya shilingi Bilioni 1.2.