Mwakyembe afanya uteuzi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameteua kamati ya watu 25 kwaajili ya kuratibu maandalizi ya michuano ya AFCON kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Akizungumza na waandishi wa habari leo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe amesema Kamati hiyo itaongozwa na yeye mwenyewe kama Mwenyekiti, wakati Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
Waziri pia amemteua Dkt. Henry Tandau kuwa Mtendaji Mkuu wa kamati hiyo. Mwakyembe amesema ni heshima kubwa kwa Tanzania kupewa uenyeji wa mashindano hayo, hivyo ni muhimu kwa Serikali kwa kushirikiana na TFF kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya michuano hiyo.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, Wakili Dk. Damas Ndumbaro, Dk. Francis Michael, Mohamed Dewji, Yusuph Omary, Ahmed Mgoyi, Khalid Dallah, Waziri wa Maliasiri na Utalii Mh. Khamis Kigwangala, Nassib Mbaga, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah, Dk. Alan Kijazi wa TANAPA, Dk James ambaye ni Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na mipango.
Wengine ni Dkt. Makakala Kamishina wa Uhamiaji, Fred Manoki, Lameck Nyambaya, William Erio, Kelvin Twisa, Ladislaus Matindi na Mama Devota Mdachi.
Waziri Mwakyembe amesisitiza kuwa mwaka 2019 si mbali hivyo ni lazima yafanyike maandalizi ya mapema na Kamati hiyo itakutana Jumamosi ijayo kwa ajili ya kupanga ratiba nyingine pamoja na kuchagua Kamati nyingine ndogondogo.