Tanzania yaombwa kususia mechi

Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo nchini, Zitto Zuberi Kabwe, ameitaka timu ya soka ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars kususia mechi na Libya, kuonyesha kutokubaliana na vitendo vya biashara ya utumwa inayoendelea Libya.

Zitto Kabwe ameyasema hayo kwa kuandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa twitter, huku akiunga mkono kauli ya mchora vikatuni maarufu Tanzania Masoud Kipanya, juu ya Tanzania kususia mechi hiyo
"Leo Masou Kipanya ameshauri Tanzania isusie mechi yake dhidi ya Libya siku ya Jumapili kuonyesha kuchukizwa na Biashara ya Utumwa. Ninaunga mkono. Tanzania isiingie uwanjani kucheza na Libya. SADC iagize nchi zake zote zirudishe mabalozi wake kutoka Libya", ameandika Zitto Kabwe.
Zitto Kabwe hakuishia hapo aliendelea kwa kuwataka watanzania wachukue hatua kuonyesha kuchukizwa na kupinga vitendo hivyo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu, vinavyoendelea nchini Libya.
"Kwanini Watanzania waliopo Dar tusichukue hatua dhidi udhalilishaji wa Waafrika? Siku ya Ijumaa tukutane ubalozi wa Libya hapa nchini kuongea na Balozi na kumpa risala yetu kupinga biashara ya utumwa inayofanyika nchini Libya, mnaonaje?", ameandika Zitto Kabwe kwenye twitter.
Hivi karibuni kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Libya baada ya kuibuka biashara ya utumwa, huku mataifa mbali mbali ya Afrika yakikaa kimya bila kutoa maamuzi dhidi ya vitendo hivyo vyenye historia mbaya hasa barani Afrika.