Saa 24 za Ndugai kuhusu wanafunzi zapata majibu

Juzi Spika wa Bunge Job Ndugai aliipa serikali saa 24 kuhakikisha inatoa taarifa kamili bungeni kuhusu kadhia wanayokutana nayo wanafunzi wanaofanya udahili wa kujiunga na ngazi ya Elimu ya juu nchini.
Agizo la Spika lilitokana na Mwongozo uliombwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Martha Mlata ambaye alieleza bunge kuwa wanafunzi wamekuwa wakihangaika vyuoni baada ya kutakiwa walipe fedha za usajili kabla ya kupewa mkopo.
Mapema leo Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewasilisha kauli ya Serikali kuhusu udahili na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2017/2018 ambapo amewaagiza wakuu wote wa vyuo vya elimu ya juu kuacha urasimu .
"Pesa imetolewa na Serikali wakuu wa vyuo acheni urasimu katika kutoa fedha kwa wanufaika wa mikopo ambao wana makubaliano na Serikali, kwani mwisho wa siku lazima atatakiwa kuurejesha mkopo huo sasa pindi utakapo msumbua kama unampa bure sio haki" amesema.
Waziri ameongeza kuwa "Jambo hili halikubaliki hata kidogo na linaleta shaka kuhusu uadilifu wa vyuo husika. Naiagiza TCU (Tume ya Vyuo Vikuu) na Kurugenzi ya Elimu ya Juu ya Wizara, kufuatilia kwa karibu mambo yote yanayopendelea vyuoni wakati wanafunzi wanaripoti na kubainisha wote wanaokiuka taratibu," amesema.
Profesa Ndalichako ametoa tamko hilo Bungeni ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Spika Job Ndugai lililotaka serikali kutoa kauli kuhusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutakiwa kutoa fedha ili wasajiliwe kabla ya kupata mikopo.