Mwakyembe aja na njia ya kuwaenzi Mashujaa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua Maonyesho ya Mashujaa na ambayo yanalenga kuonyesha namna mashujaa wa Tanganyika walipambana kupata uhuru, ambayo yatafanyika kwa muda wa mwezi mmoja katika Makumbusho
ya Taifa- Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa maonyesho hayo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kwa lengo ya kuendeleza juhudi za Uhifadhi wa Hifadhi ya Urithi Tanzania,hususani ya Ukombozi wa Afrika yanasimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo, Dkt. Mwakyembe alisema mradi huo wa kuhifadhi historia ya Ukombozi wa bara la Afrika ni muhimu kwa Tanzania kwani unaweza kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kuliko ilivyo sasa kwani inawapa nafasi wageni ya kuona mambo tofauti na yaliyozoeleka pindi wanapokuja nchini.
“Tuna mradi ambao utatupeleka mbali sana Watanzania, Afrika Kusini, Namibia, Angola hata wao wametuambia tusije shangaa sehemu hiyo ikawa inaleta watalii wengi zaidi kuliko wanaokuja kuangalia tembo na simba, urithi wa Afrika tumekabidhiwa na bara la Afrika ni wajibu wetu Watanzania kuusukuma huu mradi maana tumeshachelewa Watanzania wengi labda hawaelewi mwaka 2011 kwa kushirikiana na UNESCO tulipeleka ombi AU la mradi huu wa bara la Afrika na wakaubariki huu mradi na wakaamua makao makuu yawe Tanzania na sisi tukachagua Dar es Salaam na hapa kitajengwa kituo kikubwa kitakuwa na historia ya Ukombozi wa Afrika, sisi ndiyo viongozi wa huu mradi,” Mwakyembe
Aidha Waziri Mwakyembe ameongeza kwamba ili kufanikisha mradi huo tayari wameanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha pindi watakapojenga kituo ambacho kitatumika kuhifadhi vitu mbalimbali ambavyo vilitumika katika kipindi cha ukombozi wa bara la Afrika kuwe na taarifa nyingi kuhusu bara la Afrika.
“Tunawatumia wazee walio na historia ya ukombozi wa Afrika tumehoji zaidi ya wazee 100 na tunaendelea na hilo zoezi na tumebaini maeneo zaidi ya 200 Tanzania ambayo yanahitaji kuhifadhiwa, ni wajibu wangu kupeleka muswada bungeni ili tuyahifadhi na kuyalinda kwa kutumia sheria, Ameongeza Mwakyembe
Kwa upande wa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer alisema ni muhimu kwa bara la Afrika kuwa na maonyesho ambayo yanaelezea historia ya bara hilo ili yatumike kuelezea kizazi cha sasa na kijacho namna nchi za Afrika zilipambana kupata uhuru na wao kama EU wataendelea kusaidia miradi mbalimbali yenye lengo ya kutunza urithi wa bara la Afrika.
“Ni jambo la kujivunia kwa Umoja wa nchi za Ulaya kusaidia kufanikisha mradi huu … EU tumekuwa tukisaidia miradi mingi na hii yote ni kwa ajili ya kutunza utamaduni na urithi wa bara la Afrika, tumesaidia miradi mbalimbali nchini ikiwepo ya Olduvai na Ngorongoro na tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuendeleza maeneo ya kihistoria,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO kanda ya Afrika Mashariki na Afisa Mwakilishi wa Unesco Dar, Ann Therese Ndong- Jatta katika hotuba yake iliyosomwa na Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege alisema ni jambo zuri kuwepo na makumbusho ambayo yanaeleza historia ya bara la Afrika na yataweza kuwapa nafasi watu mbalimbali kutoka mataifa ya nje ya bara la Afrika kuona na kujifunza historia ya Afrika.
Post a Comment