Timu ya taifa ya ngumi kujipima Uganda na Kenya

Timu ya taifa ya ngumi imeingia kambini tayari kwa maandalizi ya michuano ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika April mwakani nchini Australia.
Akizungumza na EATV kocha wa timu hiyo David Yombayomba amesema wapo kwenye maandalizi na tayari timu imeshapatikana na mazoezi yanaendelea kwenye uwanja wa ndani wa taifa ambapo wanatarajia kujipima na timu mbalimbali zikiwemo kutoka nje ya nchi.
"Timu tayari ipo kambini tunafanya mazoezi kila siku kwenye uwanja wa ndani wa taifa na tunatarajia kuanza mechi za kujipima nguvu kuanzia Septemba 30 ambapo tutacheza na timu ya Ngome na baadae tutacheza na JKT", amesema Yombayomba.
Kocha huyo ambaye awali alikuwa anaifundisha timu ya Ngome, ameongeza kuwa baada ya kujipima na timu za ndani watacheza na timu kutoka Uganda pamoja na Kenya ili kuhakikisha wanapata uzoefu wa kutosha.