Madiwani wa CCM waisusia serikali

Madiwani wa jimbo la Geita wamesusia kikao cha serikali na uongozi wa mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) kufuatia kukamatwa na polisi kwa Mbunge na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Geita Mhe. Joseph Msukuma jana


Madiwani hao wamegoma kushiriki kikao cha usuluhishi kilichopaswa kufanyika leo huku wengine wakizikimbia familia zao wakiogopa na wao kukamatwa na jeshi la polisi kama ambavyo madiwani wengine walivyokamatwa kitendo ambacho kimepelekea Kamishina wa madini nchini kushindwa kutatua mgogoro uliopo kati ya uongozi wa mgodi wa Geita Gold Mine pamoja na viongozi hao na wananchi wa Geita. 
Siku ya Alhamisi ya Septemba 14, 2017 wananchi mkoani Geita walifunga barabara inayoingia katika mgodi wa GGM kushinikiza malipo ya kodi ya dola milioni 12 lakini jana Septemba 17, Mbunge wa Geita Joseph Kasheku Musukuma alikamatwa na Polisi mkoani humo, akihusishwa na tuhuma za kuhusika kwa tukio la kufunga barabara ya kuelekea kwenye mgodi wa GGM wiki iliyopita.
Jeshi la polisi mkoani Geita limethibitisha kuwa Mbunge Msukuma pamoja na madiwani sita na raia wakawaida wawili kuwa bado wanashikiliwa na polisi kwa kuratibu vurugu, katika mgodi wa Geita Gold Mine.