UNGUJA: Kituo cha Mafuta kinachomilikiwa na Bakhresa chateketea kwa moto
UNGUJA: Kituo cha Mafuta cha United Petroleum(Kinachomilikiwa na Mfanyabiashara mashuhuli Bakhresa) kilichopo katika eneo la Kinazini chaungua kwa moto mapema leo. Aidha tayari kikosi cha zima moto kimefika eneo la tukio na kinaendelea na zoezi la ukoaji.
Kituo cha United Petrolium kilichopo Kinazini mjini Unguja, kimeungua moto leo asubuhi baada ya mlipuko kutokea kwenye gari la kubebea mafuta la kampuni ya Bakhresa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amesema chanzo cha tukio hilo lililotokea leo Jumapili saa 1:30 asubuhi ni gari la kampuni hiyo ambayo ndiyo mmiliki wa kituo hicho.
Amesema dereva wa gari hilo aliyetambuliwa kwa jina moja la Ismail alitoka ndani ya gari na kufunga mipira ili kuanza kushusha mafuta.
“Alipomaliza kufunga mipira kwenye visima vya mafuta, alipanda juu ya gari ili kuweka sawa mitambo lakini alipofungua mlango wa tangi lililopo juu ya gari ulitokea mlipuko uliosababisha moto mkubwa ulioenea kituoni na kwenye baadhi ya maduka yaliopo jirani na kituo,” amesema Kamanda Ali.
Amesema hasara iliyosababishwa na moto bado haijatambulika na kwamba, kikosi kazi kinaendelea kufanya tathmini.
Kamanda Ali amesema dereva ambaye alipata majeraha amepelekwa hospitalini kwa matibabu.
Amesema moto huo umezimwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment