Manara afunguka kuhusu Omog
Uongozi wa klabu ya Simba kupitia Afisa habari wake Haji Manara umesema hauna mpango wa kumtimua kocha wao mwenye uraia wa Cameroon Joseph Omog kama watu wanavyozusha katika mitandao mbalimbali ya kijamii hivi karibuni.
Manara ameeleza hayo wakati alipokuwa anazungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mchana wa leo na kusema klabu ya wekundu wa Msimbazi haiendeshwi kwa makelele ya mitandao bali ipo makini katika utendaji kazi wake wa kila siku.
"Kabla ya mechi yetu jana dhidi ya Mwadui FC, Rais wa klabu ya Simba Bw. Salim Abdalla alikutana na kocha Omog na kumfikishia ujumbe kutoka kamati ya utendaji kuwa tuna imani naye na kumwambia aendelee kufanya kazi kwa uhuru bila ya shinikizo lolote, uongozi upo nyuma yake na unampa ushirikiano kwa kila hali", amesema Manara.
Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "Hakuna taarifa iliyotoka kwenye uongozi wala kwangu mimi kuwa imempa Omog mechi tano, hizo siyo za kweli na hatuna mpango wa kumtimua kwa sababu anafanya vizuri. Kuna baadhi ya watu wanadhani kubadilisha kocha kila mwaka ndiyo mafanikio ya timu hiyo siyo kweli ", amesisitiza Manara.
Kwa upande mwingine, Manara amesema timu ya Simba inatarajiwa kuondoka kesho (Jumanne) alfajiri ikielekea Mkoani Mwanza kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Mbao FC huku ikiwakosa wachezaji wake wawili ambao ni Said Nduda pamoja na Shomari kutokana na kuwa majeruhi.
Post a Comment