Rooney akiri kosa, ahukumiwa

Nyota wa zamani wa Manchester United Wayne Rooney amekutwa na hatia ya kuendesha gari akiwa ametumia kilevi katika kesi iliyosomwa leo kwenye mahakama ya Stockport Magistrates Kusini mwa jiji la Manchester.
Rooney alikuwepo mahakamani hapo ambapo amekutana na hukumu inayomtaka kufanya kazi za jamii kwa muda wa saa 100 pamoja na kuripoti mahakamani kwa miezi 12 huku adhabu kubwa ikiwa ni kutoendesha gari kwa miaka miwili.
Rooney alikamatwa asubuhi ya Septemba 1 akiwa anaendesha gari mitaa ya nyumbani kwake Prestbury, Cheshire ambapo vipimo vya wana usalama wa barabarani vilionesha ametumia kilevi kiasi cha 104mg.
Tayari Rooney mwenye miaka 31, ameomba msamaha kwa uongozi wa klabu yake ya Everton pamoja na mashabiki wa klabu hiyo. Imeripotiwa Eveton itamkata Rooney mshahara wa wiki mbili. Pia adhabu yake ya kutoendesha gari inaweza kupunguzwa hadi wiki 24 endapo atapata mafunzo maalum ya usalama barabarani kufikia Februari 2, 2019.