Singida United yaifikia Simba
Moja ya vitu ambavyo vinaleta mafanikio kwenye taasisi au klabu yoyote ya michezo ni udhamini mnono kutoka kwa makampuni ya kibiashara.
Hili linajidhihirisha wazi kwa klabu ya Singida United iliyorejea ligi kuu msimu huu baada ya kusota kwa miaka kadhaa katika ligi za madaraja ya chini. Singida United imeonyesha kuwa na mipango mizuri ya kupata mafanikio baada ya kufanikiwa kuwashawishi wadhamini mbalimbali kuweka mzigo.
Kwa hesabu za haraka haraka Singida United inaingiza kiasi cha shilingi milioni 700 kutoka kwa wadhamini pamoja na wadau wake. Akifafanua udhamini huo Mkurugenzi wa timu hiyo Festo Sanga amesema kampuni ya Sports Pesa inatoa milioni 250, wakati YARA wanatoa shilingi milioni 300.
Kampuni ya Puma inatoa milioni 120 wakati DTB imetoa milioni 20 kama mdau wa timu hiyo huku mdau mwingine NMB akitoa milioni 10. Jumla ya pesa hiyo ni shilingi milioni 700 ikiwa pungufu milioni 100 tu kufikia kiasi cha shilingi milioni 800 inayopata Simba kutoka SportsPesa.
Post a Comment