Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania waomba kurudi makwao
WAKATI serikali za Tanzania na Burundi zikianza utaratibu wa
kuwarudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao zaidi ya wakimbizi 6,000
wamejiorodhesha na kuomba kurudishwa nchini mwao.
Uamuzi wa wakimbizi hao umekuja wakati utekelezaji wa agizo la Rais
John Magufuli wa Tanzania na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
uliofikiwa hivi karibuni ukichukua mkondo wake.
Agizo hilo linahusisha wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye kambi mbalimbali mkoani Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alitoa taarifa hizo katika
kikao cha pamoja cha siku tatu cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
wa Kigoma na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa mitano ya Burundi
kilichofanyika Mkoa wa Makamba nchini Burundi kuanzia Julai 29, mwaka
huu.
Maganga alisema katika kikao hicho aliouongoza ujumbe wa mkoa wake na
kilizungumzia mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama, ikiwemo maandalizi
ya kuwarudisha wakimbizi wa Burundi wanaohifadhi nchini kutokana na
kujiridhisha kwamba kwa sasa hali ya ulinzi na usalama nchini Burundi ni
shwari.
Alisema pia walipata nafasi ya kuzunguka mikoa mbalimbali ya Burundi
ambako pamoja na taarifa zilizotolewa kwenye kikao hicho, pia
wamejiridhisha kwamba kwa sasa Burundi inayo amani na hivyo wakimbizi
wanaohifadhiwa nchini hawana sababu zinazowafanya kukimbia hali mbaya ya
usalama iliyokuwepo awali.
Pamoja na hilo, alisema pia Agosti 31, mwaka huu kitafanyika kikao
cha pamoja cha pande tatu kinachohusisha Serikali ya Tanzania, Burundi
na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR)
kitakachozungumzia kurudishwa nchini kwao kwa wakimbizi wa Burundi
wanaohifadhiwa Tanzania.
“Kwa sasa hakuna wakimbizi wanaopokewa hapa nchini hasa Mkoa wa
Kigoma kutokana na kuomba hifadhi kutokana na hali mbaya ya usalama
nchini mwao, tumethibitisha kwamba kigezo cha kuomba hifadhi kutokana na
hali mbaya ya usalama hakipo lakini hilo la baadhi ya raia wa Burundi
kuomba hifadhi nchini kwa kigezo cha hali mbaya ya uchumi (njaa) nchini
mwao hatuna uhakika nalo lakini vyombo vyetu vinalifanyia kazi,” alisema
Maganga.
Kwa mujibu wa gazeti la habari leo nchini Tanzania Kikao hicho mbali
ya kuhudhuriwa na mkuu wa Mkoa wa Kigoma, pia kilihudhuriwa na Balozi wa
Tanzania nchini Burundi na Mwambata wa Kijeshi katika Ubalozi wa
Tanzania nchini Burundi huku Burundi ikiwakilishwa na mikoa ya Makamba,
Ruyigi, Rutana, Cyankuzu na Rumonge.
Vyanzo vya habari zimeelelza kuwa Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya
Magharibi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Thoony Laiser alisema
wakati mkimbizi anatakiwa kurudi nchini mwake kwa mujibu wa taratibu za
kimataifa, anazo haki mbalimbali atapewa ikiwemo kuanza mtaji wa kuanzia
maisha ambapo kikao cha Agosti 31, mwaka huu kitazungumzia maandalizi
hayo.
Laiser alisema hadi sasa wakimbizi zaidi ya 6,000 kutoka kambi ya
Nyarugusu wilayani Kasulu, Nduta na Mtendeli za wilayani Kibondo
wamejiorodhesha na kuomba kurudishwa nchini mwao hadi kufikia jana huku
idadi ya wakimbizi wanaotaka kurudishwa nchini mwao baada ya kauli za
marais hao ikizidi kuongezeka. Pamoja na hilo, Laiser alisema yapo
mawasiliano baina ya idara ya wakimbizi na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
Kibondo ambayo yanayoangalia namna wakimbizi hao watakavyorudi nchini
mwao.
Post a Comment