Mawakili wa CUF- Maalim wadai mahakama haizuiwi na bunge
Wabunge wa viti maalum wa chama cha upinzani CUF nchini Tanzania,
wamefikisha malalamiko yao mahakamani na hata hivvyo wako njiapanda.
Wako njiapanda kutokana na pingamizi la maombi yao ya kusimamisha uapishwaji wa wabunge wapya walioteuliwa kuziba nafasi zao.
Wakili Kibatala alifafanua kuwa kifungu walichokitumia kufungua
maombi hayo ni sahihi huku akirejea kesi mbalimbali zilizokwisha
kuamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani akidai zilihalalisha
matumizi ya kifungu hicho.
Kuhusu hoja ya kuzuia Bunge kutekeleza majukumu yake, alidai kuwa
mahakama ndicho chombo cha kutoa haki na kwamba hakuna kanuni ya
kisheria inayoizuia kutoa haki na kwamba hakuna kanuni ya kisheria
inayoizuia kutoa haki kwa mambo yanayohusiana na Bunge na kwamba imekuwa
ikifanya hivyo.
Kuhusu kuwajumuisha wajibu maombi wengine kwenye kesi ya msingi
alidai kuwa upo uamuzi wa kuteuliwa kwa wabunge wapya uliofanyika wakiwa
tayari wameshafungua kesi ya msingi na kwamba maelezo ya jambo hilo
yako kwenye hati ya kiapo.
Waombaji hao ni Miza Bakari Haji na wenzake saba wakati wajibu maombi
ni Katibu wa Bunge, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Bodi ya Wadhamini wa CUF na wabunge wateule wanane.
Mbali na Miza, waombaji wengine katika maombi hayo ni Saverina
Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa, Riziki
Shahari Mngwali, Hadija Salum Al-Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu
Heri Sakala na madiwani Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein
Madib.
Kutokana na pingamizi hilo, mahakama ililazimika kusitisha
usikilizwaji wa maombi ya msingi hivyo kusikiliza kwanza hoja za
mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na wajibu maombi hayo ili
kuyatolea uamuzi kabla ya kuendelea na maombi hayo.
Usikilizwaji wa maombi hayo sasa unategemea uamuzi wa mapingamizi hayo utakaotolewa Ijumaa na Jaji Lugano Mwandambo.
Wabunge hao walifungua maombi Mahakama Kuu wakiomba itoe amri ya zuio
kwa Bunge ili wabunge wapya wasiapishwe, wakati wakisubuiri kesi
waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama wa chama hicho kusikilizwa.
Lakini inakabiliwa na pingamizi la awali kutoka kwa wajibu maombi,
wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali kwa madai kuwa ni batili na
kuwasilisha hoja nne kuyakosoa, jambo ambalo limefanya yabaki njia
panda.
Lakini Tume ya Uchaguzi (NEC) na Bunge waliowakilishwa na jopo la
mawakili wanane wa serikali wakiongozwa na Wakili wa serikali mkuu,
Gabriel Malata katika pingamizi lao wamewasilisha hoja tatu, moja
wakidai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa yamefunguliwa kwa kifungu
kisicho sahihi.
Walidai kuwa kifungu cha 2(3) Sheria ya Mamlaka ya Mahakama Kuu
kutumia sheria za nje hususan za Uingereza (Jala) siyo sahihi kwani
hicho kinatoa ridhaa kwa mahakama kutumia sheria za nje pale ambako
kunakuwa hakuna kifungu rasmi katika sheria za nchi.
Malata alisema walipaswa kuonyeshwa kifungu rasmi katika sheria za Uingereza kinachotumika kulingana na mazingira ya maombi yao.
Katika hoja nyingine, Malata alidai kuwa nafuu wanazoziomba haziwezi
kutolewa na mahakama hiyo kwa kuwa zinalenga kwenda kuzuia utekelezaji
wa majukumu ya kikatiba ya mhimili mwingine (Bunge).
Katika hoja ya tatu ya pingamizi hilo alidai kuwa maombi hayo ni ya
usumbufu na matumizi mabaya ya mwenendo wa mahakama kwa kuwa watoa
maombi wanaomba nafuu kwa jambo moja katika mamlaka mbili tofauti.
Post a Comment