Seneti yathibitisha balozi Green kuongoza USAID
TANZANITE BLOG
Baraza la Seneti la Marekani Alhamisi limethibitisha aliyekuwa Mbunge
Mark Green ambaye ni chaguo la Rais Donald Trump kuongoza Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
Balozi Green anachukuwa nafasi hiyo wakati ambapo uongozi wa Trump umependekeza kupunguza msaada wake na kuboresha shirika hilo.
Green alikuwa mwakilishi wa Chama cha Republikan
cha Marekani kutoka Wisconsin kuanzia mwaka 1999 mpaka mwaka 2007,
balozi wa Marekani nchini Tanzania chini ya utawala wa Rais mstaafu
George W. Bush na rais wa Taasisi ya International Republican Institute,
akijishughulisha na kutangaza demokrasia na utawala bora nje ya nchi.
Kipindi chake cha kutumikia USAID kinaanza katikati
ya mpango wa uongozi wa Trump unaolenga kupunguza bajeti kwa asilimia
31ya taasisi hiyo na ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Pia uteuzi wake umekuja wakati ambao mgogoro mkubwa
wa wakimbizi unazikabili nchi za Ulaya na mwengine wa Mashariki ya Kati
unaotokana na vita vinavyoendelea huko Syria na Iraq, balaa la njaa na
ukame katika baadhi ya maeneo ya Afrika ambayo yamewaondoa maelfu ya
wakazi kutoka katika maeneo yao.
Shirika hilo limetangaza Alhamisi raundi ya pili ya
harambee kwa ajili ya kusaidia maeneo mengine zaidi yalioathiriwa na
ukame katika nchi za Afrika.
Uteuzi wa Green umepokewa kwa shangwe kubwa na wataalamu wa maendeleo na makundi yanayotoa misaada.
Post a Comment