Ujenzi wa Daraja la Mto Momba Kuanza Mwaka Huu

1
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akielekea kukagua sehemu ambapo litajengwa Daraja la Momba litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe .Kulia ni Meneja wa Wakala wa barabara  (TANROADS)Mkoa wa Rukwa  Eng. Msuka Mkina na Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha.
2
Meneja wa Wakala wa barabara(TANROADS), Mkoa wa Rukwa  Eng. Msuka Mkina (aliyenyoosha kidole) akimwonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa tatu kulia) eneo lipakapojengwa Daraja la Momba wakati alipokagua sehemu ambapo litajengwa Daraja hilo litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.
3
Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha (Kulia) akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta Mkoani Rukwa wakati Naibu Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani alipotembelea jimboni kwake.
4
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (aliyenyoosha mkono) akifafanua kwa wananchi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta Mkoani Rukwa kuhusu  ujenzi wa daraja la Mto Momba litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.
5
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akitoa maelezo kwa wananchi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta Mkoani Rukwa kuhusu  ujenzi wa daraja la Mto Momba litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.
6
Wananchi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta Mkoani Rukwa wakifurahi mara baada ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo picha) kutoa tamko la kupatikana kwa Mkandarasi atakayejenga daraja la Mto Momba litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.
7
Muonekano wa Sehemu ambapo daraja la Mto Momba litakapojengwa. Daraja hilo litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe.
…………………………………………………………………………..
Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani amesema daraja la Mto Momba lenye urefu wa mita 75 litakalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe litaanza kujengwa  mapema mwaka huu.
Eng. Ngonyani ametoa kauli hiyo mara baada ya kukagua barabara ya Kasansa hadi Kilyamatundu na eneo litakapojengwa daraja la Momba na kusema kuwa Serikali imeshampata Mkandarasi atakajenga daraja hilo.
“Serikali imeshatoa kiasi cha sh. Bilioni tatu  fedha hizo zimetusaidia kutangaza zabuni na kumpata mkandarasi, tayari Mkandarasi wa ujenzi huu ameshapatikana na mkataba wa makubaliano ya ujenzi umeshakamilika hivyo mkandarasi atausaini rasmi hivi karibuni,” amesema Eng. Ngonyani.
Aidha, Eng.Ngonyani amemtaka Meneja Wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anatoa ajira kwa wakazi waliopo kata ya Kipeta ambapo ujenzi wa daraja hilo utafanyika.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha ameishukuru Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza ahadi ya ujenzi wa daraja hilo ambalo kukamilika kwake kutawaletea maendeleo wakazi hao kwa vile litaufungua Mkoa wa Rukwa na kuunganisha na Songwe na Katavi.
“Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili kutarahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kutoka mkoa wetu kwenda mikoa mingine inayopakana na mkoa huu na kuokoa maisha ya wananchi ambapo awali walikuwa wa wakiliwa na mamba na wengine kusombwa na maji wakati kuvuka kwenye mto huu,” amesisitiza Malocha.
Kwa upande wake meneja wa TANROADS Rukwa Eng. Msuka Mkina amewahakikishia wakazi kijiji cha  Kilyamatundu kuwa Wakala utasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na viwango na kupitia mradi huo wananchi hao watapata ajira.
“Naomba niwahakikishie wakazi wa hapa kuwa daraja hili sasa litaaanza kujengwa na nyinyi mtakuwa sehemu ya wafanyakazi katika ujenzi wa mradi huu nawaomba mtoe ushirika kwa mkandarasi pindi mradi huu utakapoanza,” amesema Eng. Mkina.
Naibu Waziri Eng. Edwin Ngonya amekamilisha ziara yake ya kukagua ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu, Bandari   na Madaraja katika Mkoani Rukwa.