RC Makonda atoa siku saba kwa DCP Mkondya
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa
Paul Makonda leo ametoa siku saba kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam DCP Lucas Mkondya kuhakikisha wizi wa vifaa vya
Magari unakomeshwa mara moja.
Akitoa maagizo hayo, Mheshimiwa Makonda
amesema wizi wa vifaa vya magari vikiwemo Vioo, Radio, Side mirrow,
Power Window,Taa pamoja na Shoo ya mbele na nyuma ya Gari vimekuwa
vikishamiri kila kukicha jambo linalowakera wananchi na kuwapa hofu ya
kuweka magari yao kwenye maegesho kwa kuhofia kuibiwa kitendo ambacho
amesema hakivumiliki.
“Sitaki kusikia watu wanaibiwa vifaa vya
Magari yao,watu wanaibiwa Vioo, Power Window,Radio, Taa,Side Mirror na
wakati mwingine wanavunja vioo vya gari na kuiba Pochi na Laptop, sasa
haiwezekani wizi wa namna hii uendelee kwenye Mkoa wangu, sasa Kaimu
Kamanda Kanda Maalumu nakuagiza na ninakupa siku saba sitaki kusikia
wizi wa vifaa vya magari ukiendelea, nataka ifikie hatua mtu aweze
kuegesha Gari lake na kulikuta likiwa salama” Alisema Makonda.
“Mwananchi yoyote atakaeibiwa na
akapeleka taarifa Polisi na hatua za kisheria zichukuliwe atoe taarifa
kwangu bahati nzuri wananchi wana namba zangu, haiwezekani Mwananchi
anajikusanya na kununua gari alafu anaibiwa watu wanaiba vifaa vyake,
wizi wa namna hii nasema Mwisho ndio umefika leo," Alisisitiza Makonda.
Aidha Makonda ameagiza Maduka na Vijiwe
vyote vinavyouza vifaa vya Magari kujisajili mara moja iliviweze
kutambulika na Serikali.
“Kinachoshangaza ni kwamba hawa wanaoiba
wana vijiwe vyao ambapo wanauza hivyo vifaa, ukienda Kariakoo, Magomeni
na pia Temeke (Keko) kuna vijiwe ambavyo ukienda kule unakuta kifaa
kilichoibiwa kwenye Gari lako kipo mtaani kinauzwa” Aliongeza Makonda.
Akipokea Maagizo hayo, Kaimu Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam DCP Lucas Mkondya amesema kuwa
maagizo hayo yanaanza kutekelezwa leo ambapo msako utaanza leo
kuhakikisha Genge la wezi wa vifaa vya magari vinasambaratishwa.
Aidha amewaagiza Makamanda wa polisi
Temeke, Ilala na Kinondoni kuanza utekelezaji wa maagizo hayo kuanzia
leo na kuwataka wote wanaouza vifaa vya wizi kujisalimisha mara moja kwa
Jeshi la Polisi.
Post a Comment