MAHAKAMA YA RUFAA KENYA YATUPILIA MBALI KESI YA NASA
Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imebatilisha uamuzi wa mahakama
uliokuwa umezuia kampuni ya Al Ghurair ya Dubai kuchapisha karatasi za
kupiga kura za urais.
Mahakama hiyo ya pili ya ngazi ya juu nchini Kenya Jumanne imesema
kuwa Mahakama ya chini ilifanya makosa kwa kutoa amri kusitisha
uchapishaji huo kwa sababu ya kuwashirikisha wananchi.
Majaji walitoa uamuzi kuwa kushirikishwa wananchi katika mchakato huo
wa kutoa tenda sio sharti katika manunuzi ya moja kwa moja, utaratibu
ambao ulitumiwa na tume ya uchaguzi katika kuipa mkataba huo Al Ghurair.
Pia waliikosoa Mahakama hiyo kwa kushindwa kutambua kuwa muda ulikuwa finyu mno kuweza kushughulikia kutoa tenda nyingine.
Hata hivyo, majaji wa mahakama ya rufaa walikubaliana na wale wenzao
wa Mahakama ya chini kutupilia mbali madai kuwa Rais Kenyatta alikutana
na maafisa wa Al Ghurair na alitumia nafasi yake ya urais kuwapa tenda
hiyo.
Mahakama hiyo, wamesema, ilikuwa sahihi kuweka msimamo kuwa vipande
vya magazeti haviwezi kutosheleza kuthibitisha kwamba Rais alikutana na
wakurugenzi wa kampuni hiyo.
“Makala hizo zinabakia kuwa uvumi mpaka pale mwandishi atapoweza
kutokea mahakamani na kuhojiwa juu ya ukweli wa habari hizo,” wamesema.
Post a Comment