Wabunge na Wafuasi wa CHADEMA wakosa dhamana
Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Morogoro, imeshindwa kutoa dhamana kwa Wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Peter Lijualikali wa Kilombero pamoja na Suzani Kiwanga wa Mlimba na washtakiwa wengine 34 wa Chama hicho.
Dhamana hiyo imeshindikana kupatikana baada ya kutokea mvutano wa kisheria baina ya Mawakili wa Serikali na upande wa utetezi, juu ya kiapo cha kupinga washtakiwa hao kupatiwa dhamana.
Wabunge hao wakiwa na washtakiwa wengine 34 wamefikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoani humo , wakishtakiwa kwa makosa nane ikiwemo Kula njama ya kutenda kosa, Mkusanyiko usio wa halali, Kufanya Ghasia, uchochezi wa kutenda kosa shtaka ambalo linawakabili Mbunge Peter Lijualikali na Suzani Kiwanga, Shtaka la tano ni kuchoma nyumba mali ya Serikali yaKijiji, sita Uharibifu wa mali zenye thamani ya Milioni 100.8 huku shitaka la saba na nane likiwa ni uharibu wa mali kwa makusudi, makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda Novemba 26 , mwaka huu katika kata ya Sofi Wilayani Malinyi kwenye uchaguzi mdogo wa marudio ya Udiwani.
Baada ya upande wa Washtakiwa kuwasilisha maombi ya kuomba dhamana, Upande wa Mawakili wa Serikali nao waliendelea na msimamo wao, na kuiomba Mahakama izuie dhamana hiyo, hadi hapo nao watakapopitia hati iliyowasilisha na upande wa utetezi ya kutaka washtakiwa hao wapatiwe dhamana kwani ni haki yao ya msingi
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, Haklimu Ivan Msaki alichukua maamuzi ya kughairisha tena kesi hiyo hadi Desemba 6 ya Mwaka huu, ambapo watakutana tena kujadili juu ya kiapo kilichokuwa kimewasilishwa na upande wa mawakili wa Serikali, kupinga washtakiwa hao kupatiwa dhamana.
Post a Comment