USAFI WA MAZINGIRA DODOMA SASA KILA WIKI, WATAKAOKAIDI FAINI 50,000 AU JELA MIEZI 6


Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro  (kushoto) akifuatilia usafishaji wa barabara na mitaro katika barabara ya Dodoma-Singida wakati wa zoezi la usafi wa Mazingira unaofanywa kila Jumamosi ikiwa ni Kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge.
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Uhuru Manispaa ya Dodoma Ally Kheri (kulia) akishiriki zoezi la usafi wa Mazingira katika Mtaa wa Barabara ya 8 katikati ya Mji wa Dodoma wakati wa zoezi la usafi wa Mazingira unaofanywa kila Jumamosi ikiwa ni Kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge.
........................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imepanga kutumia askari wa Mgambo 30 watakaokuwa wanafanya doria katika viunga vya Mji ili kudhibiti watu wanaochafua mazingira kwa kutupa taka ovyo ikiwa ni namna mojawapo ya kuhakikisha mji huo unakuwa safi wakati wote ikizingatiwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya Nchi.

Hatua hiyo inafuatia kampeni ya usafi wa mazingira iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge ya kufanya usafi siku ya Jumamosi kila wiki.

Akizungumza wakati wa zoezi la usafi mwishoni mwa Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema askari Mgambo 30 waliofuzu mafunzo wako tayari na kwamba Manispaa inatarajia kuanza kuwatumia wiki hii ya kwanza ya mwezi Desemba.  


Aliwashauri wakazi wa Dodoma na wageni kujiepusha na utupaji wa taka ovyo, na kwamba atakayebainika na kuthibitika kufanya hivyo atatozwa faini kati ya Shilingi 50,000 hadi 300,000 kulingana na mazingira ya tukio papo hapo na endapo atashindwa kulipa atatumikia kifungo cha miezi sita gerezani.