Nikihama chama wataniua

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam, Issaya Mwita amefunguka kuwa kamwe hafikirii kuhama Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kusema kwamba hafikirii kuhama chadema kwani familia yake itateketezwa kwa mapanga na wananchi akiwepo yeye pia.
Akizungumza leo asubuhi kupitia kipindi cha EABreakfast,  ndani ya East Africa Radio, Mwita amesema kwamba amekitumikia Chadema kwa muda mrefu ikiwepo kutumia fedha zake binafsi kwenye kukijenga chama hivyo hadhani kama anaweza kuhamia chama kingine kwani hata madaraka aliyonayo anaamini yanamtosha kabisa.
Mwita amesema kwamba amesikitika sana kuona kuna baadhi ya watu waliohama vyama na kuongeza kwamba yeye ameaminiwa na wana Dar es salaam ndiyo maana akapewa dhamana kubwa ambayo ni kubwa kuliko hata nafasi ya Waziri.
"Nchi hii tumeanza kuitumikia tangu tupo majeshini. Hatukuwahi kununuliwa, lakini nawashukuru wana Dar es salaam kwa kuniamini pia nafasi niliyonayo ni kubwa. Nahama Chadema naenda wapi na nikienda huko nitafanya kazi gani? Najua kuna 'Cheap' Politics ambayo inafanyika ili kubomoa chama chetu lakini sisi tunaamini hapa tutavuka jambo hili na tutafika pazuri". Meya Mwita
Mwita amesema kwamba sifa moja ya kabila analotoka siyo watu wa kuyumbishwa hivyo siku atakapobadili msimamo ndiyo siku ambayo ataipoteza familia na yeye mwenyewe.
"Nipo ndani ya chama hiki tangu 1999. Nimekijenga kwa nguvu na pesa zangu. Hivyo naanzaje kufanya upumbavu kama huo. Nikuambie siku nikifanya uamuzi huo utasikia mama yangu amekufa, kaka zangu na hata mimi mwenyewe, Siku nikihama labda wanihamishie mbinguni lasivyo wataniua. Unataka mimi nife....aaah siwezi". amesema Mh. Mwita
Aidha, Mh. Mwita amesema kwamba aina yake ya kuliongoza jiji la Dar es salaam imekuwa tofauti sana kwani ameamua kuwa mkimya ili kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo suala la kupiga kelele halitakuwa na tija kama hakutakuwa na maendeleo.