Mkuu wa wilaya 'ashangazwa
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mwl. Herman Kapufi ameshangazwa na jitihada binafsi zilizofanywa na wachimbaji wadogo katika kata ya Nyarugusu wilayani hapo baada ya kushirikiana na serikali ya Kata kufanikisha ujenzi wa shule.
Wachimbaji wadogo kwenye Kata ya Nyarugusu na Serikali ya kijjiji na kata hiyo wameshirikiana kuchangia ujenzi wa madarasa manne na ofisi 2 za walimu kwenye Shule ya Msingi Tologo.
Mkuu wa wilaya alifika shuleni hapo kujionea jitihada za kuboresha miundombinu ya shule ya Tologo ambayo madarasa yake yaliharibiwa na mvua zilizoambatana na upepo hali iliyopeekea kubaki darasa moja tu.
Kiongozi wa wachimbaji hao Bw. Evarist Pascal alimweleza mkuu wa wilaya kuwa kutokana na kuwepo kwa hali ambayo ilisababisha wanafunzi kusomea madarasa ambayo yalikuwa yameezuliwa na mvua walionelea ni vyema wakichangia ujenzi huo hili watoto wapate sehemu nzuri ya kujisomea.
Bw. Evarist amemwambia mkuu huyo wa wilaya kuwa ujenzi wa madarasa hayo pamoja na ofisi za walimu umegharimu kiasi cha Sh, Milioni 56 ambazo zimechangwa na wachimbaji wadogo kutoka katika machimbo ya dhahabu ya Nyarugusu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Mwl. Herman ameeleza kushangazwa na uzalendo ambao umeoneshwa na wachimbaji hao kwa kuchangia ujenzi wa miundombinu hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano kwenye ujenzi wa Zahanati ya kitongoji cha Tologo ambapo hadi sasa wachimbaji hao wamefyatua tofali 3,000.
Post a Comment