DED KALIUA : TUMEANZA KULIMA KOROSHO KAMA ZAO JINGINE LA BIASHARA .
NA TIGANYA VINCENT
RS-TABORA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imesema imeanza ulimaji wa zao la Korosho ili kuongeza katika mazao ya biashara litakaloungana na pamba na tumbaku ikiwa ni hatua ya kuandaa malighafi kwa ajili ya viwanda na kuongeza mapato yake.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua John Pima wakati wa ufungaji wa mafunzo ya Madiwani yaliyokuwa yakiendeshwa na Chuo cha Serikali za MItaa Hombolo ili kuwajengea uwezo viongozi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Alisema kuwa tayari washapanda miche zaidi ya 1350 katika vijiji 10 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ikiwa ni sehemu ya mashamba darasa kwa ajili ya wananchi kujifunza kwa wale wanaohitaji kulima zao hilo.
Pima aliongeza kuwa hivi karibuni wamepokea kilo 80 mbegu za korosho ambazo pia watazipanda katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya kuendelea na zoezi hilo la kilimo hicho.
Alisema kuwa udongo wa Kaliua unafaa kwa ajili ya zao la Korosho jambo ambalo linatoa fursa nyingine kwa wakazi wake kuwa na zao jingine linaloweza kuwapatia fedha.
Pima aliwaomba Madiwani kuhakikisha wanafikisha taarifa kwa wananchi katika maeneo yao juu ya uwepo wa mbegu hizo ili waweze kujitokeza na kuanza kulima zao hilo,
Alisema kuwa wanataka kutumia fursa ya uzuri wa ardhi yao katika kulima mazao mbalimbali za biashara kwa ajili ya kuhakikisha wakazi wao wanakuwa na uhakika wa kupata fedha kutokana na uuzaji wa mazao ya biashara,
Pima alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa wanaongeza mapato yao ya ndani kutokana na makusanyo za mazao mbalimbali ya biashara ili hatimaye waweze la kuelekea katika kujitegemea katika miaka michache ijayo.
Akifunga mafunzo ya siku tatu yakikuwa yakiwajengea uwezo madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Kaliua , Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliwaagiza viongozi hao kuanza kuwahamasisha wakulima juu ya ulimaji wa korosho, alizeti na pamba kwa ajili ya kupata malighafi za viwanda.
Alisema kuwa kilimo hicho cha korosho ni sehemu ya utekeleza wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ambapo aliwashauri viongozi kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakulima kuanza kulima mazao kama vile korosho kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Post a Comment