Sitawapa muda - Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama Cha ACT Wazalendo, Mhe. Zitto Kabwe amefunguka na kusema hawezi kuwapa muda watu ambao wamekuwa wakitumwa kutaka kuhamisha mjadala kuhusu wahusika halisi ambao wamefanya shambulio la risasi kwa mbunge Lissu
Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama Cha ACT Wazalendo, Mhe. Zitto Kabwe.
Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa twitter ameweka wazi msimamo wake huo wa kutoyumbishwa na watu hao ambao wameanza kusambaza taarifa mbalimbali kuhusu Zitto Kabwe na kusema hizo ni ajenda wanazofanya kutaka kumtoa kwenye mstari wa sakata hilo jambo ambalo amedai hawezi kulipa nafasi kabisaa.
"Hizi ni propaganda za dola ili kuhamisha mjadala kuhusu wahusika halisi wa shambulio la risasi dhidi ya Mbunge Tundu Lissu. Sitawapa muda" alisisitiza Zitto Kabwe
Mbali na hilo Zitto Kabwe amesema kuwa watu ambao wamefanya shambulio hilo la kinyama dhidi ya Mbunge Tundu Lissu wamelenga kuwatisha wabunge na wanasiasa ambao wamekuwa mstari wa mbele kuongea mawazo yao na kusema jambo hilo halitakiwa kupewa nafasi linatakiwa kulaaniwa ili washindwe kuendelea na mambo ambayo si ya Kitanzania na wala hayajawahi kuzoeleka nchini.
"Watu waliomfanyia shambulio Lissu wamelenga kututisha kuzungumza mawazo yetu na mitazamo yetu, na kama tutaamua kukaa kimya watashinda, hivyo hatutakiwi kuwapa nafasi hiyo watu hawa, tunatakiwa kupinga dhidi ya udhalimu huu" alisema Zitto Kabwe
Mbunge Zitto Kabwe amekuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya kinyama na kikatili ambavyo vimeanza kutokea Tanzania, kuanzia kuuawa kwa baadhi ya viongozi mbalimbali na askari polisi Kibiti Pwani mpaka katika shambulio lililompata Mbunge Tundu Lissu siku ya Alhamisi Septemba 7, 2017 mjini Dodoma baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Post a Comment