Singida United kuja kivingine

Klabu ya soka ya Singida United inaendeleza jitihada za kuhakikisha inakamilisha maboresho ya uwanja wa Namfua uliopo mjini Singida ili ianze kuutumia kama uwanja wake wa nyumbani msimu huu.
Mkurugenzi wa timu hiyo Festo Sanga amethibitisha kuwa wanaendelea na ukarabati wa uwanja huo na matarajio yao hadi mwezi Desemba uwanja huo utakuwa tayari kwa matumizi ya mechi zao za nyumbani.
"Tunaendelea kuboresha uwanja wetu wa Namfua ili kuondoa yale mapungufu yaliyokuwepo na tunatarajia kuutumia msimu huu kwani hadi mwezi Desemba utakuwa tayari", amesema Sanga.
Uwanja wa Namfua ulikosa baadhi ya vigezo vya kutumika mwanzoni mwa msimu huu kutokana na sehemu ya kuchezea "Pitch" kutokuwa na ubora unaohitajika. Hivi sasa Singida United inatumia uwanja wa Jamhuri Dodoma kama uwanja wake wa nyumbani na leo itakuwa dimbani ugenini kucheza na Stand United ya Shinyanga.