CHADEMA yatoa tamko kumuombea Lissu kesho
Baraza la vijana CHADEMA (BAVICHA) limewataka watanzania wote kwa ujumla hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza siku ya kesho (Jumapili) katika maombi ya Tundu Lissu kwa madai wamekamilisha taratibu zote za kisheria juu ya jambo hilo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu (BAVICHA) Taifa, Julius Mwita kupitia ukurasa wao maalum wa Facebook wa chama hicho baada ya kupita siku ya moja tokea Kamishna Kanda maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa kuzuia kufanyika kwa maombi hayo yaliyopangwa kufanywa kwenye uwanja wa TP, Sinza Jijini Dar es Salaam kwa kuwa hiyo siyo sehemu ya maombezi.
"Kupitia kamati ya maandalizi, BAVICHA inapenda kuwaambia Watanzania wote ambao watapenda kuhudhuria maombi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuwa maandalizi yote muhimu yameshafanyika kwa ajili ya kuhakikisha shughuli hiyo ya kiimani inafanyika kama ilivyopangwa", amesema Mwita.
Julius Mwita aliendelea kwa kusema mpaka sasa wameshafuata taratibu zote za kisheria ambazo zimewaelekeza kutoa taarifa kwa mamlaka za kiserikali hususani Jeshi la Polisi
"Hadi sasa jeshi hilo halijatuandikia barua ya kutuita ili kujadiliana nao kuhusu kufanikisha shughuli hiyo, tunaamini kuwa hawana pingamizi lolote la kiutaratibu kama ambavyo sheria inaelekeza. Tumefuatilia kwa kina kuhusu kauli za Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambazo zimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo ikidhaniwa kuwa amezuia shughuli hiyo ya maombi, na tumebaini kuwa ZPC Mambosasa hakueleweka vyema", amesema Mwita.
Pamoja na hayo, Mwita ameendelea kwa kusema "Tumejiridhisha tena kuwa taarifa tuliyopeleka kwa jeshi la polisi kama sheria inavyoelekeza, tukiwataarifu kuhusu maombi hayo, haikutaja wala kuzungumzia maandamano bali watu wa dini mbalimbali zilizopo nchini wanaoguswa na tukio la Lissu na maumivu anayopitia hospitalini, watakutana na kuomba sala au dua ili Mwenyezi Mungu afanye uponyaji kwa mgonjwa wetu", amesisitiza Mwita.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu (BAVICHA) Taifa, Julius Mwita amesema maombi hayo yatafanyika kesho (Jumapili) katika uwanja wa Tip, Sinza darajani jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 8:00 mchana.
Post a Comment