"Sina mashaka na Kamusoko"- Dkt. Bavu

Daktari wa mabingwa watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, Edward Bavu amefunguka na kudai hana wasiwasi wowote na kiungo wa timu hiyo mwenye uraia wa Zimbabwe, Thabani Kamusoko baada ya kumaliza kupatiwa matibabu yake kiufasaha.
Thabani Kamusoko.
Dkt. Bavu amebainisha hayo kupitia ukurasa maalum wa timu hiyo instagram, baada ya Kamusoko kupata maumivu kwenye mguu wake wa kulia wakati akiwa uwanjani na kusababisha kutolewa nje ya uwanja kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa na muamuzi wa mchezo huo, dhidi ya Njombe Mji FC katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo.
"Sina shaka na Kamusoko tena, jana jioni amefanya mazoezi vizuri, ni jukumu la benchi la ufundi kuamua kama anaweza kuwa sehemu ya kikosi kitakachoanza”, ameandika Dkt. Bavu.
Timu ya Yanga inashuka dimbani jioni ya leo kuvaana na Majimaji FC katika uwanja wao wa nyumbani wa Majimaji mjini Songea huku ikiwa na pointi nne kibindoni mpaka sasa hivi.