"Sikuwa nimejipanga"- Linah

Msanii wa bongo fleva, Linah Sanga amefunguka na kudai hakuwa amejipanga kwa kipindi hiki kuwa na mtoto ila anamuomba Mungu isiwe kigezo cha yeye kupotea katika muziki ili aje kuwa mfano kwa wasanii wenzake wa kike wanaogopa kubebea ujauzito.
Msanii wa bongo fleva, Linah Sanga.
Linah amebainisha hayo kupitia kipindi cha FRIDAY NIGHT LIVE 'FNL' kutoka EATV baada ya kuwepo imani kwa baadhi ya watu wakidai msanii akioa, akiolewa hata akijifungua na mtoto mara nyingi hawezi kuendelea kufanya vizuri katika kazi zake kwa kuwa majukumu ya ulezi yanaongezeka na kupelekea kupotea katika 'industrial' ya muziki.
"Nina muomba Mungu usiku na mchana nisije kupotea katika 'game' kwa sababu ya uzazi, ili iwe mfano hata kwa wengine ambao watakuja nyuma yangu, labda wanaogopa kuzaa kwa kufikiri watapotea. Ila mimi nafikiri ni jinsi mtu mwenyewe anavyoishi na mashabiki zake", amesema Linah.
Pamoja na hayo, Linah ameendelea kwa kusema "Sikuwa nimejipanga kupata mtoto katika kipindi hiki ila nilikuwa na-wish nipate ujauzito nizae lakini sikufahamu ni lini itanitokea hivyo. 'So' kipindi kile nilichokuwa na-wish nikawa kila nikijaribu haingii, nikajisahau na kujikuta imekuja hata sikutarajia, lakini kwa kuwa nilikuwa nina uhitaji nikasema hakuna neno. Japo nilishauriwa vitu vingi sana mwanzoni lakini nikasema hapana kwa kuwa nimetaka kuzaa acha nifanye hivyo", amesisitiza Linah.
Kwa upande mwingine, Linah amesema kwa anajipa mapumziko katika kufanya kazi zake na kuwataka mashabiki zake wamvumilie mpaka mwakani (2018) katika miezi ya mwanzoni ndipo atakapoachia kazi yake mpya.