Polisi yakamata vijana 14 leo
Jeshi la Polisi nchini Uganda limewakamata vijana 14 wa kundi la 'Jobless Brotherhood' kwa tuhuma za kufanya maandamano kupinga marekebisho ya katiba kuhusu ukomo wa urais.
Tukio hilo limetokea leo mchana katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala, ambapo vijana waliokamatwa wamepelekwa katika kituo kikuu cha polisi, wamefanya maandamano hayo huku wakisambaza vipeperushi vyenye ujumbe wa kupinga kitendo hicho na kuita 'watu wabinafsi'.
Akizungumza na waandishi wa habari Mbunge wa nchini humo Muhhamad Nsereko ambaye ni miongoni mwa watu wanaopinga suala hilo, amesema vijana hao wamechukuliwa kwa ajili ya mahojiano hapo kesho, na wataendelea kufanya hivyo kwa manufaa ya taifa lao.
“Katiba haitabadilishwa, haturudi nyuma kwa hili licha ya kukamatwa, wanatutaka tuwe wazalendo na kuitetea nchi yetu, tusiogopeshwe , tuendelee na safari kuijenga nchi yetu”, amesema Nsereko.
Wabunge nchini Uganda wameanza kujadili mchakato wa kubadilisha katiba itakayomruhusu Rais Yoweri Museveni kubakia madarakani kwa muda mrefu zaidi, kitendo ambacho kimeonekana kupingwa vikali na baadhi ya wananchi.
Post a Comment