"Ndege iliyombeba Lissu niliita mimi" - Turky
Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky amefunguka na kusema CHADEMA ndiyo imelipa gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya na kusema yeye aliwadhamini wakati huo kwa kuwa hawakuwa na fedha taslimu za kulipa
Salim Hassan Turky ametoa ufafanuzi huo leo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Mbunge huyo ndiye aliyelipia gharama za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Kenya kwa matibabu taarifa ambayo imetolewa na Spika wa Bunge jambo ambalo CHADEMA wamelipinga na kusema Spika anapotosha umma juu ya jambo hilo.
"Nataka kuiweka Tanzania sehemu salama na ya ukweli, maneno mengine si sawa kurushiana tusifanye tukio la Lissu kutaka kufanya siasa mimi binafsi tukio la Lissu limesonenesha sana na kunisikitisha mimi ni binadamu ambaye naamini kuna kuzaliwa na kufa, mimi nilitumia uwezo niliojaliwa na Mungu nikatafuta ndege kwa 'flight link' ambao ni ndugu zetu tunafanya nao biashara sana wakakubali kutusaidia kwa dolla 9,200, ile ndege mimi ndiyo niliita kwa kukubaliana na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kwamba nisimamie mambo hayo baadaye wao waje kurejesha na ndicho kilichotokezea" alisema Turky
Aidha Turky aliendelea kueleza kuwa walipofika nchini Kenya siku ya pili walipaswa kuwa ametoa fedha hizo lakini haikuwa hivyo mpaka leo Septemba 14, 2017 majira ya saa sita mchana alipowasiliana na wahusika aliambiwa kuwa CHADEMA walikuwa wameshalipa hizo fedha.
Mbali na hilo Turky amesema kuwa kauli ambayo Spika wa Bunge Job Ndugai ameisema leo bungeni haikuwa na tatizo kwani alikuwa amesema yeye ndiye amelipa hiyo fedha lakini CHADEMA wangekuja kuirudisha kwake, jambo ambalo anadai kama leo wasingeweza kulipa CHADEMA basi angelipa yeye fedha hizo kwa watu hao halafu yeye angekuja kumalizana na CHADEMA.
Pia katika kauli ambayo ametoa Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa amesema kuwa fedha hizo za ndege iliyombeba Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Nairobi nchini Kenya imelipwa na Watanzania ambao walikuwa wanachangia fedha za matibabu kwa Lissu pamoja na CHADEMA wenyewe na si mbunge wa CCM.
Post a Comment