MUUGUZI WA SIKONGE LAWAMANI KWA UZEMBE ULIOSABABISHA KIFO CHA MTOTO MWAKA 2015

Na Tiganya Vincent
Sikonge
Muuguzi na walinzi katika Hospitali ya Wilaya ya Sikonge wanachunguzwa kwa kusababisha kifo cha mtoto wa Hadija Abdallah mnamo Novemba 2015 kilichotokana na uzembe wa kukataa kumuongezea damu.
Uamuzi huo umetolewa jana mjini Sikonge na  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akisikiliza kero mbalimbali za wakazi wa wilaya hiyo , Mkazi huyo alisema kuwa mtoto wake alilazwa katika Hospitali hiyo mnamo tarehe 11 Novemba 2015 na kuandikiwa dawa mbalimbali ikiwemo kuongezewa maji.
Hadija akisimulia tukio lilivyotokea alisema kuwa wakati akiwa anangoja mtoto wake aongezewe maji  ndipo Muuguzi wa zamu alimweleza kuwa chupa ya maji moja aliyopata haitoshi na kumwambia ampe shilingi 5,000/- ili amuongezee chupa nyingine mbili.
Alisema kuwa pamoja na kumlipa fedha hizo Muuguza huyo alikuwa akichelewa kumbadilishia chupa ya maji(drip) na kusababisha mtoto wake kukaa muda mrefu bila huduma hiyo.
Hadija aliongeza vitendo hivyo vya Muuguzi vilivyofanya hali ya  mtoto wake kuwa mbaya na ndipo alipoamua kwenda kwa Daktari na kueleza kuwa mwanae anaupungufu wa damu na kuagiza aongezewe damu lakini Muuguzi huyo alidai hakuna damu na anapaswa kutafuta mtu wa kumuongezea mtoto wake damu.
Alisema kuwa kwa kuwa alitambua kuwa mume wake alikuwa alichangia damu kwa hiari aliamua kuwaonyesha Muuguzi kadi yake lakini walikataa na ndipo alipochukua jukumu la kumupigia simu ili aje lakini alipofika getini walizi walimzuia kuingia Hospitalini.
Aliongeza wakati akiendelea kumsubiri mumuwe apewe ruhusa  ndipo mtoto wake alipopoteza maisha na Wauguzi walipobaini hilo walijifanya kuwa karibu naye na kuanza kumsaidia na walinzi wakaamua kumruhusu mumewe.
Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Tabora ameuagiza Uongozi wa Wilaya ya Sikonge kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kufanya utambuzi wahusika wa tukio na uchunguzi wa kifo cha mtoto huyo na kuwachukulia hatua kali watakaobainika kusababisha.
Alisema kuwa ikibainika kuwa kifo cha mtoto yule kilitokana na uzembe wahusika waliokuwa zamu wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Mwanri alisema Serikali haiwezi kuvumilia watumishi wachache wanaoshindwa kuwajibika au wale wanaozembea na kusababisha matatizo kwa wananchi na kusababisha Serikali kupakwa matope kwa uzembe wa watumishi wachache.
Alisema kuwa mtumishi asiyependa kuwahudumia wananchi kwa kiwango bora , mlango uko wazi aende kufanya kazi nyingine na sio kuendelea kusababishwa Serikali kupakwa matope kwa uzembe wake.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora baada ya kumaliza zoezi la kusikiliza kero za wakazi wa Sikonge anatarajia kuendelea na Wilaya nyingine.