MANJI SITAMBUI KUVULIWA UDIWANI.


Mfanyabiashara Yusuf Manji ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 9, 2017 kuwa yeye bado ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu na kudai kuwa hatambui kuvuliwa udiwani kama ilivyotangazwa na Mstahiki Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo September 6, 2017.

Manji ametoa malalamiko hayo, kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo katika kesi hiyo ambayo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai upelelezi haujakamilika na Manji kudai ameona habari kupitia gazetini kuwa amevuliwa udiwani.

Amedai kama ni kweli amevuliwa Udiwani hatambui, kwani ana miezi 2 yupo gerezani na serikali inatambua kwamba yeye ni Diwani.

"Vikao vya awali vya udiwani wa Halmashauri ya Temeke nilikuwa nahudhuria kwa kuwa naheshimu Mahakama na kwa uzito wa hii kesi sikutaka kupeleka hata maombi ya dhamana Mahakamani. Mahakama imuagizie DPP na aiambie Halmashauri ya Temeke kwamba wamenikamata na ndio sababu ya kutohudhuria vikao. Kama wanataka nihudhurie DPP aombe remove order nitolewe gerezani ili niende kwenye vikao.”

Pia Manji amedai kuwa kama hilo haliwezekani, basi wamuandikie barua itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua pia.

"Ninachotambua mimi ni Diwani wa Mbagala Kuu na kama nimevuliwa au sijavuliwa udiwani sitambui. Tayari nimetumia fedha zangu mwenyewe zaidi ya Tsh. Milioni 70 sio za Halmashauri kwa ajili maendeleo ya wananchi wake.”

Aidha, amedai kuwa hiyo kesi ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande wake wa kesi tu, kwani yeye amechaguliwa na wananchi na anawasaidia.

Awali kabla ya kuelezwa hayo, Wakili wa utetezi Seni Malimi alidai kuwa wanatarajia kuwasilisha maombi ambayo ni ya siri katika tarehe ijayo.

Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Huruma Shaidi akautaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo, ambapo kesi imeahirishwa hadi September 18, 2017.