DC MTATURU AHIMIZA UMOJA,UPENDO NA KULINDA AMANI


Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akihutubia waumini wa dini ya kiislam mara baada ya  ibada ya swala ya Eid El Hajji iliyofanyika kijiji cha Mwau Kata ya Mang’onyi wilayani humo.
mt (2)
Baadhi ya waumini walioshiriki swala ya Eid El Hajji wakimsikiliza mgeni rasmi  mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu ambaye hayupo pichani.
mt (4)
MKUU wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu ameungana na waumini wa dini ya kiislamu katika swala ya Eid El Hajji katika kijiji cha Mwau kilichopo Kata ya Mang’onyi wilayani humo.

Akihutubia mara baada ya ibada hiyo Mtaturu amewaasa waumini hao kuendelea kuilinda amani  iliyopo kwa kuwa ndio msingi mkuu wa kila jambo ikiwemo maendeleo na ibada.

Aidha amewataka kuwa wamoja,kupendana na kuishi kama ndugu bila ya kuangalia misingi ya dini wala  itikadi za vyama vyao.

Alisema serikali ina amini kuwa waumini wakifuata mafunzo na imani za dini zao watakuwa raia wema na watasameheana pale wanapokeseana.

“Ndugu zanguni tuidumishe na kuilinda amani tuliyonayo,bila ya kuwa na amani hatuwezi kufanya shughuli zozote za kimaendeleo,hatuwezi kushiriki  ibada kama hivi,amani ndio kila kitu kwetu,”alisema Mtaturu.

Alisema ili kuilinda amani kila mmoja amuheshimu mwenzie bila ya kuangalia tofauti ya kabila,dini wala chama na kusisitiza kuwa siasa sio uadui na uwepo wa vyama vingi ni kuonyesha namna nchi ilivyo na demokrasia.

“Waumini wenzangu tusiifanye siasa kuwa ni adui,uchaguzi ulishaisha hivyo kwa sasa tunapaswa kuwasaidia wananchi kusukuma maendeleo,hapa katikati tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakitoa kauli za kuwagawa wananchi na kuwachonganisha na serikali yao sisi tusifuate kauli zao,zinaonyesha ulimbukeni walionao na kudhoofisha maendeleo,”alisema mkuu huyo.

Alisema walioanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa hawakumaanisha viwepo vyama vya kukwamisha maendeleo hivyo wanasiasa wanawajibu wa kuacha siasa chafu zinazorudisha nyuma maendeleo ya wananchi ili nchi iweze kusonga mbele.

Akizungumzia kuhusu maendeleo wilayani humo amewahamisha wananchi kulima kilimo cha kujitosheleza ili wapate chakula cha kutosha na kuweka bayana mkakati wa wilaya wa kuja na zao la korosho ambapo kwa msimu huu watagawa bure miche laki 5 kwa wananchi.

Kwa upande wake mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA)wilaya ya Ikungi sheikh  Salum Ngaa alimshukuru mkuu huyo kwa kujumuika nao katika ibada hiyo na kuwahimiza waumini kufanya matendo mema yaliyoaswa na Mungu.

Alisema Hijja ni miongoni mwa nguzo za uislam hivyo imelazimishwa kuitimiza na malipo yake ni makubwa kwa Allah hivyo waislamu wanapaswa kuifanya sikukuu hiyo kuwa kwa ajili ya kufanya yale wanayofanya mahujaji waliopo hijja.

Katika ibada hiyo mh Mtaturu amechangia bati bandari(bati 16)mifuko 10 ya saruji baada ya kukuta kuna ujenzi wa madrasa ya vijana ya kujifunzia  unaendelea na  umefikia hatua ya upauaji ambapo pamoja nae waumini wengine nao wameunga mkono na kuchanga sh laki 327,950 taslimu huku ahadi ikiwa ni sh 30,000,mifuko ya saruji 7 na bati 14.