DC Kigamboni aweka wazi utaratibu huu wa eneo la 'Show Room' ya magari kwa wafanyabiashara wa magari


Akizungumza jijini Dar es Salaam na wafanyabiashara hao Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Hashim Mgandilwa ameeleza kuwa lengo la kuwapeleka wafanyabiashara hao katika eneo hilo la Kisarawe II Kigamboni ni kuwaeleza namna watakavyomilikishwa na serikali ina mpango gani na eneo hilo.
Akieleza jinisi watakavyo wamilikisha wafanyabiashara hao DC Mgandilwa amesema watawapa maeneo hayo bure kwa muda wa miaka mitatu bila malipo ila watalazimika kulipa kiasi cha shilingi laki tatu kama dhamana ya kuonesha nia, kisha baada ya miaka mitatu wataanza kulipa kodi ya nusu dola (1250) kwa mwezi kila baada ya miezi sita.
DC Mgandilwa ameongeza kuwa wafanyabiashara hao wakitaka kukodi maeneo hayo watalazimika kulipia kiasi cha shilingi 30000 kwa mita mraba moja ndani ya miezi mitatu, lakini pia wakitaka kununua kwa mwaka watalazimika kulipa 35000 kwa mita mraba moja ndani ya miaka mitatu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Property International Limited Halim Zaharani amesema eneo walilotenga kwa ajili ya shughuli hiyo ya yadi ya kuuzia magari ni mita za mraba 750,000 na wameweka ziada ya mita mraba zaidi ya 300,000.
Naye mmoja wa wafanyabiashara waliofika eneo hilo Salim Chicago amepongeza kuanzishwa kwa mpango huo wa yadi ya pamoja ambao ameeleza kuwa utawarahisishia wateja kuwa sehemu moja ambayo inatambulika na uwepo wa aina mbalimbali za magari, ambapo amebainisha kuwa mfumo huo wa kuwa na eneo maalum la uuzaji unatumiwa na nchi nyingi zilizoendelea duniani ikiwemo Dubai, Japan na Singapore.
Uwepo wa eneo hilo ni ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Kampuni ya Property International LTD, eneo hilo lipo umbali wa Kilomita 16 kutoka daraja jipya la Mwalimu Nyerere na Kilomita 10 kutoka Kibada Senta na miundombinu muhimu ya kijamii kama barabara, maji, umeme vipo katika mkakati wa uendelezaji.