WAZIRI MKUU AMPA SIKU 15 MWEKA HAZINA WA SIKONGE, APATE MAELEZO YA KUTOKUSANYA MAPATO
*Ataka apate maelezo kwa nini ameshindwa kukusanya mapato
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya
Sikonge, Bw. Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia
80 ya makusanyo ya ndani.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017)
wakati akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.
“Nataka maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80
ya makusanyo ya halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC wamefikisha
asilimia 112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini
wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato
kwa maeneo mliyoshindwa kufanya vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa
fedha. Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.
Alipopewa nafasi ya kujieleza, Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia
76.7 na wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu
uliopita, hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni
mwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo,
washirikiane na watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala
ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao.
Jana, mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu
alizitaka Halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini
zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na
Serikali.
“Halmashauri zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega
DC. Nataka taarifa za halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni
kwa nini hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni
asilimia 80,” alisema.
Taarifa ya mkoa huo inaonyesha makusanyo kwa kila Halmashauri ni kama
ifuatavyo:- Tabora Manispaa asilimia 64.1; Nzega Mji (asilimia 112); Nzega
Wilaya (asilimia 80.8); Igunga (asilimia 64.6); Tabora (asilimia 77.3); Sikonge
(asilimia 76.7); Urambo (asilimia 70.9) na Kaliua (asilimia 91.5).
Pia amezitaka Halmashauri zote zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa
kutumia mfumo wa kielektroniki. “Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike
kwa mfumo wa kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo, zitumie
makusanyo ya mwaka jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona risiti za
kuandika kwa mkono zinatumika,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora
uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika
wilaya hiyo ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya
mapato.
“Hapa Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa
TRA katika kila Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani,
watendaji wa vijiji na watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,”
alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.
Post a Comment