SERIKALI YAMALIZA SINTOFAHAMU YA TANI 3,700 ZA TUMBAKU
Serikali imefanikiwa
kumaliza sintofahamu ilikuwepo baina ya wakulima na wanunuzi wa tumbaku
mkoani Tabora juu ya uwepo wa tani 3,700 zilizokosa soko.
Tani 3,700 zilikuwa
zimekosa wanunuzi kwa sababu hazikuwa na mkataba kati ya wakulima na
wanunuzi na hivyo kuhitaji utatuzi wa haraka wa Serikali ili kuinusuru
tumbaku hiyo.
“Tumefanikiwa
kuongea nao na tutauza zile tani 3,700 kwa wanunuzi,” alisema Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa na kuamsha shangwe ukumbi mzima.
Waziri Mkuu alitoa
ahadi hiyo jana jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati akizungumza na
wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini,
chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa
Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Aliwashukuru wanunuzi
kwa kukubali kumaliza tatizo hilo kwani litaleta ari mpya kwa wakulima
na kuwafanya wajipange vizuri kwa msimu ujao. “Makampuni ya ununuzi
yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU watafuatilia na tumekubaliana nao
kuwa tutafanya kazi pamoja,” alisema Waziri Mkuu.
Kufuatia sintofahamu
hiyo, wiki iliyopita, wakazi wa mkoa huo waliomuomba Mheshimiwa Rais,
Dkt. John Pombe Magufuli aingile kati ili kuwanusuru na adha ya zao hilo
kukosa soko. Naye akawaahidi wananchi hao kwamba suala hilo
atalikamilisha Waziri Mkuu.
Mapema, Mkuu
wa Mkoa wa Tabora, Bw. Aggrey Mwanri wakati akiwasilisha muhtasari wa
taarifa ya mkoa huo alisema katika masoko ya tumbaku yanayoendelea, kuna
tatizo la tumbaku kukosa wanunuzi kwani hapakuwa na mkataba kati ya
wakulima na wanunuzi.
“Tumbaku
inayofikia kilo milioni 3.7 kwa sehemu kubwa ililimwa kwa ufadhili
wa WETCU Ltd, kwa fedha ambazo zilikuwa ziende APEX. WETCU walinunua
pembejeo na kuwapa wakulima waliokuwa chini ya vyama sinzia, na sasa
haina wanunuzi. Tunaomba ulisemee hilo ili tupate ufumbuzi wa suala
hili,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mbunge wa Urambo, Mheshimiwa
Margareth Sitta aliiomba Serikali ikubali kuliangalia suala hilo la
tani za ziada 3,700 kwani wakulima wamejaza tumbaku majumbani mwao na
kwenye maghala.
“Wakulima
wetu wanahitaji kuuza hii tumbaku ili wapate fedha za kuanzia msimu
ujao wa kilimo. Lakini pia tunaomba liangaliwe suala la upangaji
madaraja ya tumbaku, wasaidiwe kukabili bei isiyotabirika na kutatua
ukosefu wa soko la uhakika,” alisema Mama Sitta.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.
Post a Comment