Wakurugenzi andaeni mazingira bora kwa Ajira mpya – Waziri Simbachawene.

Nteghenjwa Hosseah, Kibakwe.
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuandaa mazingira rafiki kwa watumishi wapya wanaopangiwa katika Halmashauri zao.
 
Simbachawene ameyasema hayo ikiwa ni wiki moja tangu kutangaza ajira mpya za Walimu wa Masomo ya Hisabati na Sayansi wapatao 3,081 wa ngazi ya Shahada na Stashahada ambao wamepangiwa kwenye Halmashauri mbalimbali Nchini.


Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msangambuya wakati wa Ziara yake ya Kikazi Wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe Mhe. Simbachawene amesema watumishi wengi wapya wanakatishwa tamaa na mazingira mabovu wanayoyakuta katika Halmashauri zao na hali hiyo huwatia hofu ya kuendelea kukaa katika maeneo hao.


Unakuta mtumishi anafika Halmashauri malipo yake hayajaandaliwa zaidi ya mwezi mzima, kisha anapangiwa kwenye Kata mbayo hata hajawahi kuifahamu hapo awali na hapewi hata maelekezo ya ziada ya namna ya kufika katika Kituo chake na unakuta wenyeji wake katika Kata na Shule hawana taarifa za ujio wa mtumishi huyo hivyo mtumishi anahangaika mpaka anakosa ari ya kufanya kazi katika kituo chake kipya alisema Simbachawene.


“Ninahitaji Kila Halmashauri kuandaa Malipo stahiki kwa ajili ya walimu wanaoendelea kuripoti hivi sasa katika maeneo mbalimbali, Usafiri wa kuwapeleka katika vituo vyao vya Kazi, mapokezi stahiki kwa uongozi wa Kata pamoja Shule sambamba na kuhakikisha anapata makazi bora ya kuishi katika eneo lake jipya la Kazi”.


Sitaelewa Halmashauri ambayo itashindwa kuzingatia maagizo haya kwa namna yeyeote ile na ntaendelea kufuatilia mazingira ya mapokezi ya watumishi hawa, sitaki mtumishi yeyote ashindwe kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa sababu ya mazingira magumu anayokutana nayo wakati wa kuripoti kazini, Aliongeza.