Marekebisho Sheria Madini: TMAA yafutwa, leseni zasitishwa
Wizara ya Nishati na Madini imetangaza
mabadiliko katika sekta ya madini baada ya kupitishwa kwa sheria mpya
ijulikanayo kama ‘The Written Laws Act, 2017’ iliyoanza kutumika rasmi
Julai 7, iliyopelekea marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010.
Marekebisho yaliyofanyika ni pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Madini pamoja na kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA).
Wakati akitangaza mabadiliko hayo leo
jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. James
Mdoe, amesema pia kufuatia mabadiliko hayo ada ya malipo ya mrabaha
kutoka asilimia 4 kwa madini ya metali hadi 6%.
“…Kuongezeka kwa malipo ya mrabaha
kutoka 5% kwa madini ya almasi na vito hadi 6%. Aidha, kupitia
marekebisho ya sheria ya fedha na kodi hivi sasa kila mtu au kampuni
inayotaka kusafirisha madini nje yatakaguliwa na kuthaminishwa pamoja na
kulipa ada ya ukaguzi kwa 1% ya thamani ya madini anayosafirisha,” amesema na kuongeza.
“Pia mchimbaji mdogo anayeuza
madini kwa madalali atakatwa 5% ya thamani ya madini ambayo itakusanywa
na broker au dealer kupelekwa TRA.”
Aidha, Prof. Mdoe ameeleza kuwa, pamoja
na kufutwa kwa TMAA Ofisi za Madini za Kanda pamoja na watumishi wake
wasio kuwa na tuhuma wanaendelea na ajira zao kwa kuwa ni watumishi wa
serikali.
“Wafanyakazi hao wataendelea
kukusanya maduhuli ya serikali yanayotokana na madini, kukagua migodi ya
wachimbaji na miradi yote ya wazalishaji dhahabu,” amesema.
Pia, amesema katika kipindi hiki cha
mpito kabla ya tume ya madini haijaundwa shughuli zote zitafanyika chini
ya usimamizi wa Kamishna wa Madini. Hali kadhalika serikali
imesimamisha utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji madini hadi tume
itakapoundwa na kuanza kazi rasmi.
Post a Comment