TAARIFA YA ZIARA YA PIERRE NKURUNZINZA NCHINI TANZANIA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe.
Pierre Nkurunziza leo tarehe 20 Julai, 2017 amefanya ziara ya Rasmi ya
Kiserikali ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Ziara hiyo imefanyika katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera ambapo
Mhe. Rais Nkurunziza amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na
kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake katika eneo la Lemela na baadaye mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyofanyika Mjini Ngara.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika uwanja wa Posta ya zamani Mjini Ngara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na
Mkewe Mama Janeth Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nkurunziza kwa kukubali
mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano
itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na
kidugu na nchi ya Burundi hususani katika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tanzania ni ndugu zako na Watanzania ni ndugu wa watu wa
Burundi, umekuja kwa mazungumzo ya kiuchumi, tumezungumza mambo mengi
ya kuimarisha biashara kati Tanzania na Burundi, katika takwimu za mwaka
2016 biashara kati ya Tanzania na Burundi ilikuwa na thamani ya
Shilingi Bilioni 116.5, kiwango hiki ni kidogo kwa nchi ya Burudni
ambayo ina watu zaidi ya Milioni 10 na Tanzania ambayo ina watu zaidi ya
Milioni 52” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania
inaendelea na juhudi zake za kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa
(Standard Gauge) ambayo itaunganisha bandari ya Dar es Salaam
na nchi za Burundi na Rwanda na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais
Nkurunziza kuwa reli hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa
Tanzania na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Nkurunziza kwa juhudi
zake za kusimamia amani nchini mwake na ametoa wito kwa wakimbizi wa
Burundi ambao bado wapo nchini Tanzania kuitikia wito wa Rais wao
aliyewataka warudi nchini Burundi ili wakaendelea kujenga Taifa lao kwa
kuwa hali ni shwari.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kusitisha utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao
ili utaratibu huo usitimiwe kama kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Nkurunziza amemshukuru Mhe. Rais Magufuli
kwa mwaliko wake na amesema Tanzania na Burundi ni ndugu na majirani
ambao uhusiano na ushirikiano wake ulianza hata kabla ya uhuru.
Mhe. Rais Nkurunziza ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania
kwenda kufanya biashara Burundi na wafanyabisahara wa Burundi kuja
Tanzania bila wasiwasi na amebainisha kuwa hali ya Burundi ni shwari
kwani hata wakimbizi waliokimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita
wameanza kurejea nchi Burundi kwa hiari yao na wanaendelea na shughuli
zao kama kawaida.
“Tunataka kuwajulisha wenzetu Watanzania na Warundi
wenzetu ambao walikimbilia Tanzania, Burundi ya leo ni nchi yenye amani,
tunawaalika Warundi wenzetu, kaka zetu na dada zetu ambao walikimbilia
hapa Tanzania, warudi nchi kwao tujenge nchi yetu iwe na amani ya
kudumu.
Tunapata faraja kwamba Warundi wenzetu ambao walikimbilia
Tanzania miaka miwili iliyopita ambao wanafikia idadi ya 150,000
wameanza kurudi Burundi bila ya kupitia Shirika la Wakimbizi Duniani
(UNHCR), kwa hiyo tunasema wote rudini nyumbani” amesema Mhe. Rais Nkurunziza.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mawaziri watano na
Mhe. Rais Nkurunziza ameongozana na Mawaziri watano ambao pamoja na
viongozi wengine wa taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki
mazungumzo rasmi.
Mhe. Rais Nkurunziza amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini Burundi.
Kesho tarehe 21 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara
yake Mkoani Kigoma ambapo ataweka jiwa la msingi la ujenzi wa barabara
ya Nyakanazi – Kibondo na barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na
kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
20 Julai, 2017
Post a Comment