MUSEVENI AWAONYA WANASIASA,WAANDISHI WA HABARI UGANDA
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaonya wanasiasa na waandishi wa
habari kuwa watakabiliwa na nguvu zote za dola endapo watajihusisha na
vitendo vya uchochezi dhidi ya serikali.
Museveni amedai ni uchochezi kwa makundi hayo kueneza chuki kuhusu azimio la kubadilisha katiba.
Pia amesema kwamba wakati mwafaka utakapofikiwa, atafanya maamuzi yake kuhusu katiba ambayo wengi hawatapendelea.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti Alhamisi kuwa baada ya
kimya cha muda mrefu, hatimaye rais wa Uganda Yoweri Museveni
amezungumzia kuhusu harakati zilizopo kubadilisha katiba hatua ambayo
wachambuzi wa kisiasa wanasema inalenga kumsaidia kusalia madarakani.
Akionekana mwenye hasira, Museveni amesema kwamba amekuwa akisikia
watu wakizungumzia kuhusu katiba kubadilishwa, lakini hana muda kuulizia
kwa kina wanazungumzia nini, akisisitiza kwamba atakapofanya maamuzi
yake, wanaojadili swala hilo hawatafurahia.
Museveni alifanyia marekebisho katiba ya Uganda mwaka 2005 na kuondoa kizuizi cha mihula miwili kwa kiongozi wa taifa.
Tangia kipindi hicho, amekuwa akiwania urais na kusalia madarakani
japo wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakidai kwamba hufanya udanganyifu
mkubwa katika hesabu za kura.
Lakini hivi sasa, umri unamzuia kuwania tena ifikapo mwaka 2021,
kwani atakuwa ametimiza miaka 76 wakati katiba inaweka kizuizi kuwa
miaka 75.
Wakati Museveni akieleza azimio hilo la kuifanyia marekebisho katiba,
waziri wake wa uekezaji Anite Everline amedai kupokea vitisho vya
kuuawa kwa kuwa yuko mstari wa mbele katika kafanikisha azimio hilo.
“Wamenitishia maisha na hata kutishia maisha yangu kwamba wataniua.
Lakini nimewaeleza kwamba nitakufa leo, nao watakufa kesho,” amesema
waziri huyo.
Wanasiasa wa upinzani nao wameapa kuhakikisha kwamba ibara ya 102b
haifanyiwi mabadiliko kuondoa kizuizi cha umri kwa wagombea urais
Post a Comment