MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAM AKABIDHIWA KOMPYUTA 50.
KISIGINO HABARI
Posted on: July 14th, 201
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda amepokea
Computer 50 zenye thamani ya shilingi Million 85 kutoka katika kampuni
ya ulinzi ya TAMOBA kama namna ya kuunga mkono utendaji kazi mzuri
unaofanywa na Ofisi hiyo.
Upatikanaji wa Computer hizo umekuja ikiwa ni sehemu ya shauku na
utafutaji wa Mheshimiwa Makonda kwa ajili ya kuongeza tija na ufanisi
katika kuwahudumia wananchi wa Dar es Salaam, ambapo itakumbukwa hivi
karibuni Mheshimiwa Makonda alifanya mkutano na Watumishi wa sekta ya
Ardhi wa Manispaa zote na moja ya kero kubwa iliyo bainishwa kuwasumbua
wananchi ni namna ya kupata kibali cha ujenzi jambo lililomkera
Mheshimiwa Makonda.
Kucheleweshwa kwa huduma ya namna hii kwa wananchi huchochea utoaji
Rushwa na ujenzi holela bila vibali unaosababisha Serikali kupoteza
kodi ya viwanja na kodi zingine zinazohusiana na ardhi.
Aidha amesema kuwa wananchi wamekuwa wakipata kero mbalimbali ikiwemo
ile ya kupewa kibali na manispaa kisha wakaja watu wa zima moto
wakakuzuia kuendelea kwa ujenzi sababu hawana taarifa, huku wakati
mwingine ukimalizana na watu Zimamoto wanakuja watu wa OSHA nao
wanakuzuia usiendelee na ujenzi.
Hivyo basi badala ya hivi vitengo husika nane kuwa sehemu moja (one
stop center) badala yake vimetawanyika na kuwa kero na usumbufu kwa
wananchi hasa wanaotaka kufuata taratibu.
kutokana na sababu zote hizo Mheshimiwa Makonda ameamua kutengeneza
mfumo mpya utakaomwezesha mwananchi kutokwenda kupanga foleni Manispaa
yoyote ile anapotaka kibali cha ujenzi badala yake anaweza kutuma kwa
njia ya mtandao na vitengo vyote vinane vikapokea taarifa hizo kwa
wakati mmoja na kumfanya kila mwenye kitengo chake kuwajibika kwa wakati
pasipokuwa na kisingizio cha kupoteza taarifa za wateja, urasimu na
hata lugha mbaya kwa wananchi wanaotaka huduma ya Serikali.
Aidha mfumo huo utamwezesha Mkuu wa Mkoa kuona nani anakwamisha
utendaji ili hatua za haraka zichukuliwe na mwananchi apate huduma ya
haraka.
Mfumo huu pia utamwezesha mwananchi kutuma kero inayohusu huduma ya
ardhi popote alipo na ikapatiwa ufumbuzi pasipo yeye kuhangaika.
Mkuu wa Mkoa ameahidi pia kuwapatia Pikipiki 50 watendaji wa idara ya
ardhi ili waweze kufanya safari za haraka kwenda kwenye migogoro ya
ardhi pale inapoibuka kabla ya madhara makubwa kutokea.
“Nataka ifike mahali Mwananchi yoyote Yule bila kujali
kipato chake akiomba kibali cha ujenzi apatiwe ndani ya mwezi mmoja,
haiwezekani mtu anatuma maombi ya kupata kibali cha ujenzi anazungushwa
na hatimae anakata tamaa na mwisho wa siku anajenga bila kibali na
kusababisha ujenzi holela.” aliongea Makonda.
Kwa hiyo ndio maana nikaona twende kwenye mfumo wa kupata kibali cha
ujenzi ndani ya muda mfupi na Serikali kupata mapato. Nikimaanisha ndani
ya mwezi mmoja unatosha kupitia taarifa na kupitia maombi yao ili
kamati ya mipango miji ifanye kazi yake ndani ya wakati.” alisisitiza
Makonda.
Sanjari na hayo Mkuu wa Mkoa ameushukuru uongozi wa kampuni ya
TAMOBA kwa kutimiza ndoto aliyonayo na kueleza kuwa sasa ni wakati wa
wataalamu kukamilisha mfumo ili wananchi waanze kupata huduma ya kisasa
na aina yake.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TAMOBA Balozi Mstaafu
Francis Mndolwa amesema kuwa wameamua kutoa zawadi hizo kwa mkuu wa mkoa
ili kusaidia kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wakazi wa
jiji la Dar es salaam huku akionyesha kushangazwa na watanzania
wanaoingiza chuki na ubinafsi katika kazi nzuri anayoifanya Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bwana Joseph Kimisha amesema kuwa
kampuni yao inafarijika na namna ofisi ya mkuu wa mkoa inavyoshughulikia
kero za wananchi kwa ufanisi na kueleza kuwa wataendelea kushirikiana
na ofisi hiyo bega kwa bega
Post a Comment