Jeshi la polisi latangaza oparesheni maalumu ya kuwabaini wezi wa vifaa vya magari.
Jeshi la polisi kanda maalum ya dar es
salaam limetangaza operesheni maalum ya kuwabaini wezi wa vifaa vya
magari ambapo wafanyabiashara wote ambao wanauza vipuri vya magari
vilivyotumika wanatakiwa kuonyesha nyaraka za kuingiza bidhaa zao hapa
nchini pamoja na risiti za kodi walizolipia kodi na kama watashindwa
kufanya hivyo wataunganishwa na kundi na wezi wa vifaa vya magari.
Operesheni hiyo imetangazwa na kaimu
kamanda wa polisi wa kanda hiyo Lucas Mkondya wakati akitangaza
operesheni hiyo kwa umma ambapo amesema maduka mengi ya vifaa vya magari
vimekuwa vikitumika kama sehemu ya kuuzia vitu vya wizi.
Aidha kamanda huyo amesema watahakikisha
wanakomesha mtandao wote wa wezi wa magari na tayari wametuma kikosi
maalaum cha polisi nje ya nchi kwenda kubaini mtandao huo wawezi wa
magari.
Baadhi ya wananchi wamepongeza mpango
wa kuwabana wezi wa vifaa vya magari kwani wizi huo umekuwa sugu na watu
wamekuwa wakiishi bila ya kuwa amani na magari yao.
Vilevile Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam limefanikiwa kukamata silaha moja aina ya Shotgun ikiwa
na risasi tano ndani ya magazine maeneo ya Pemba Mnazi wilaya ya
Kigamboni Jijini humo.
Kamanda Lucas Mkondya ameeleza kuwa
mnamo tarehe 16 Julai walikuta silaha hiyo yenye namba za usajili TZ CAR
3421 ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana katika maeneo ya ufukwe
wa bahari ya hindi wakati askari wakiwa doria, ambapo silaha hiyo
imehifadhiwa kituo cha polisi Kigamboni na upelelezi unaendelea.
Katika Matukio mengine Kaimu Kamanda wa
Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Lucas Mkondya ameeleza kuwa mnamo
tarehe 11 Julai mwaka huu limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu kwa
wizi wa magari huko Ukonga akiwemo Adamu Hamisi dereva na mkazi wa
Kwamkolemba Moshi Bar Ukonga, Adamu Karubya-Dereva na Mkazi wa
Vingunguti, na George Andrew wakiwa na magari mawili ya wizi.
Magari hayo yaliyokamatwa ni pamoja na
lenye namba za usajili T.730 CTJ aina ya Toyota Rav 4 rangi ya blue
ambayo imefutwa Chasis namba, lingine ni gari namba T.212 DEF Toyota IST
rangi nyeusi ambayo iliibiwa mnamo tarehe 1 mwezi wa 5 huko kipunguni
Moshi Bar.
Aidha gari ya aina ya Toyota IST
lilikamatwa huko Magomeni likiwa tayari kubadilishwa rangi yake ya awali
ili kuwa na rangi nyeupe ikiwa pamoja na kubandikwa namba nyingine
T.827 BZL.
Post a Comment