Yanga yajinadi

Kocha mkuu wa Yanga George Lwandamina amesema mechi yao ya raundi ya 10 ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mbeya City itakuwa ngumu lakini watapambana washinde.
Lwandamiza amesema ni lazima wajitahidi washinde mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa Uhuru leo jioni ili wasiachwe mbali na mahasimu wao Simba katika mbio za ubingwa.
“Tunaingia kwenye mchezo mgumu, lakini tutapigana tushinde, Mbeya City ni timu nzuri na kwa sababu imefungwa mechi mbili mfululizo leo watakuwa wakali sana, lakini tutajitahidi tushinde,”amesema Lwandamina.
Kwa matokeo ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata Simba jana dhidi ya Tanzania Prisons yanainyima Yanga nafasi ya kukaa kileleni hata ikishinda leo. Simba sasa ina alama 22 ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga yenye alama 17. Ili kuipiku Simba, Azam FC yenye alama 19 inahitaji kushinda mabao 13-0 dhidi ya wenyeji Njombe Mji FC leo jioni.
Mechi nyingie ya kukamilisha mzunguko wa 10 leo itapigwa Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar wakiwakaribisha ndugu zao Kagera Sugar.