*WILAYA YA UBUNGO LEO 28/12/2017 YAZINDUA KAMPENI YA UHAMASISHAJI WA UNYWAJI DAWsA ZA KINGATIBA ZA MABUSHA NA MATENDE*
Leo hii Kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya chini ya Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mh.Kisare Makori imezindua rasmi zoezi la uhamasishaji wa kampeni ya kutoa Kingatiba ya dawa kwa ajili ya magonjwa yaliyosahaulika ya Matende na Mabusha.
Akifungua kikao hicho maalum kwa ajili ya uzinduzi Mh.Mkuu wa Wilaya amesema kwa mujibu wa takwimu inaonyesha watu bil.1 duniani wameathirika na magonjwa haya na kuna makisio kuwa watu bil.2 wako hatarini kuambukizwa.
Akisisitiza umuhimu wa watu kuitikia wito katika kupata dawa hizi ambazo zitaendelea kutolewa kuanzia leo 28/11/2017 mpaka 3/12/2017 amesema wananchi wajitokeze kwani dawa hizi ni kwa ajili ya kuimarisha afya na kutuepusha na maradhi hayo ambayo yana madhara makubwa kwetu.
Akiongea kuhusu dhana potofu kuwa dawa hizi zina madhara Mkuu wa Wilaya amesema maneno hayo si ya kweli kwani dawa hizi zimepitia hatua zote za uchunguzi na kuthibitika ni salama kwa afya ya binadamu na hazina madhara yoyote,hivyo wajitokeze kwa wingi kunywa dawa hizi katika vituo vilivyowekwa ambapo ni maeneo ya mikusanyiko kama masokoni,vituo vya afya vya umma na binafsi,makanisani,miskitini .
Katika hatua nyingine Mratibu wa zoezi hili kwa upande wa Ubungo ndg.Abdala amezitaja sababu zinazopelekea magonjwa haya kuwa ni minyoo midogo midogo inayoathiri mfumo wa maji na damu ya binadamu ,vimelea hivyo husambazwa na mbu.
Aidha ameeleza kuwa kampeni inaanza rasmi tarehe 28/11/2017 hadi 3/12/2017,idadi ya walengwa wanakadiriwa kuwa 1,141,956 ambapo jumla ya vituo vya kutolea huduma ni 136 vyenye watoa huduma 272.
Shime wananchi tujitokeze katika vituo tupate dawa hizi ili kuepuka madhara yanayotokana na magonjwa haya.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO MANISPAA YA UBUNGO
Post a Comment