Usafiri Dar es salaam kuboreshwa

Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam Sipora Liana na Meya wa wa jiji hilo Isaya Mwita wamefanikiwa kusaini mkataba wa ushirikiano na jiji la Humberg Ujerumani katika sekta mbalimbali.
Pande hizo mbili, zimekubaliana kushirikiana katika uboreshaji wa huduma za usafiri wa umma na shughuli za kukuza utalii katika Jiji la Dar es Salaam. Maeneo mengine ni mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo pamoja na upangaji wa miji.
Mkataba huo kati ya majiji hayo dada umesainiwa Novemba 14, mwaka huu jijini Hamburg na Meya Mwita na Meya Olaf Scholz wa Hamburg na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana.
Mkataba wa awali wa uhusiano huo ulitiwa saini mwaka 2010 na Adam Kimbisa na Ole Van Beust waliokuwa mameya wa majiji hayo katika kipindi hicho.
Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wapo nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi ambapo mbali na kusaini mkataba huo pia wameshiriki mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Bonn.