WATUMISHI WANOLEWA KUDHIBITI MATUMIZI MABAYA YA GHARAMA ZA UCHAGUZI

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Jaji Francis S.K Mutungi amewataka watumishi kutoka ofisi yake kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi ili kuleta weledi katika kazi.

Hayo ameyazungumza wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa kwa ajili ya watumishi watakaoshiriki katika usimamizi wa  utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Gharamaza Uchaguzi  kwa Vyama vya Siasa na wagombea yaliyofanyika Jana na Leo katika ukumbi wa Bunge Jijini Dar esa Salaam.

“Chapeni kazi na kuwa vinara wa kusimamia gharama za uchaguzi na maadili ya Vyama vya Siasa  ili kubaini wagombea ambao hawafuati matakwa ya   sheria   ” amesisitiza Jaji Mtungi.

Naye Bi Piencia Kiure, Msajili Msaidizi wakati akitoa mada juu Elimu ya maadili ya Vyama vya Siasa ,amewasisitiza watumishi kuendelea na utamaduni wa kufanya kazi kwa weledi.

Sheria namba 6 ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 kupitia Amri ya Gharama ya uchaguzi inaweka wazi viwango  vya juu vya matumizi kwa wagombea, kudhibiti matumizi ya fedha zinazotumika wakati wa uchaguzi kuanzia katika mchakato wa uteuzi, kampeni na kupiga kura ili kuweka uwanja sawa wa kisiasa na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Sheria hii hubainisha wajibu wa Mgombea na Chama cha Siasa kujaza fomu maalumu za gharama za uchaguzi ili kubainisha bajeti yake ambayo ni mapato  na vyanzo vya mapato na kurejesha katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  ndani ya siku saba baada ya uteuzi wa wagombea unaofanywa na Tume ya uchaguzi .

Fomu maalumu ya kubainisha marejesho ya matumizi ya uchaguzi inayoambatana  na kumbukumbu na stakabadhi za malipo hujazwa na mgombea na kurejeshwa kwenye chama chake ndani ya siku sitini baada ya uchaguzi, chama cha siasa kina wajibu wa kuiwasilisha fomu hiyo kwenye ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ndani ya siku 180 baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi

Hata hivyo ukiukwaji wa sheria hii unaambatana na adhabu kali ambayo hutolewa kwa chama ambacho kitashindwa kuwasilisha mapato na matumizi ya kila mgombea ambayo ni pamoja na kufutiwa kushiriki uchaguzi endapo kitashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha.

Usimamizi wa Sheria ya gharama za Uchaguzi katika uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe  Novemba 26 mwaka huu ni mwendelezo  wa usimamizi wa sheria hii ambao hufanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  wakati wa uchaguzi wa Urais, Wabunge na Madiwani. Kwa mara ya kwanza sheria hii ilianza kutumika katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010