Wapinzani wakamatwa

Wafuasi kadhaa wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, wamekamatwa jana Jumapili mjini Lubumbashi walipokuwa wakihudhuria mkutano wa maandalizi ya kuwasili kwa kiongozi wa chama cha UDPS, Felix Tshisekedi, katika katika mji huo.
Kwa mujibu wa viongozi wa serikali , watu waliokamatwa walikuwa barabarani, wakati ambapo upinzani unadai kuwa polisi walikwenda kuwatafuta kwenye makao makuu ya chama cha UDPS.
Wakati wa tukio hilo, Kamishna wa Polisi wa Mkoa huo, Jenerali Paulin Kyungu, alikuwa akiongoza operesheni kwenye makao makuu ya UDPS.
Kwamujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Haut-Katanga, Pande Kapopo, watu waliokamatwa walikuwa mitaani, wakati ambapo sheria iliyowekwa miezi kadhaa iliyopita inasema maandamano yanaruhusiwa kwa idhini ya kiongozi wa manispaa ya mji .
Umoja wa Mataifa leo umetoa wito kwa serikali ya DRC kuwaachilia huru mara moja wafuasi wa upinzani waliokamatwa siku ya Jumapili katika mji wa Lubumbashi, kusini mashariki mwa nchi hiyo.