Tarehe rasmi ya kuanza masomo Vyuoni
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Eleuther Mwageni amesema wanafunzi ambao tayari wamekidhi vigezo na kupitishwa kujiunga na elimu ya juu wanatakiwa kuripoti chuoni ili kuanza masomo ifikapo Oktoba 30.
Prof. Mwageni ameyasema hayo leo wakati anatoa ufafanuzi juu ya tarehe ya kufunguliwa kwa vyuo kutokana na mkanganyiko ambao wameupata baadhi ya wanafunzi kuhusu muda sahihi wa masomo kuanza kwa mwaka wa masomo 2017/18 hususani wale ambao wameomba nafasi kwenye awamu za pili na tatu za Udahili.
“Tarehe ya Kalenda ya masomo haijabadilika iko palepale ambayo ni Oktoba 30 wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/2018”, amesema Mwageni.
Aidha Prof. Mwageni ameeleza kuwa zaidi ya wanafunzi 450,000 tayari wameshapata vyuo hivyo kinachosubiriwa katika awamu ya tatu ni kupitisha wanafunzi wengine 12,000 ili kufikia malengo ambayo ni wanafunzi 57,000.
Awamu ya tatu ambayo ilianza Oktoba 18 hadi 22 imefikia hatua nzuri ambapo vyuo vinawasilisha TCU majina ya waombaji ambao vimewapitisha ili tume iweze kujiridhisha kisha wanafunzi waliochaguliwa katika awamu hiyo wajiunge na vyuo na waanze masomo kwa wakati.
Mapema mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alishauri TCU iweke utaratibu wa wanafunzi kuomba nafasi chuoni moja kwa moja ili waende vyuo wanavyotaka wao tofauti na awali ambapo zoezi la kupanga vyuo lilikuwa linasimamiwa na Tume hiyo ya Vyuo Vikuu TCU.
Post a Comment