Mjadala wa Lissu ufungwe

Mkuu wa jeshi la polisi nchini, IGP Simon Sirro ametaka mjadala ufungwe mara moja kuhusu
 sakata la mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kupigwa risasi na watu wasiojulikana mnamo 
Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo leo akiwa ziarani jijini Mbeya wakati akizungumza na vikosi vya 
ulinzi na usalama ambapo amewaonya wanasiasa kuacha kuuendeleza mjadala wa jambo hilo 
na waliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake.

Mbali na hilo IGP Sirro amewataka wananchi hususani wa mkoa wa Mbeya, kuacha tabia ya 
kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutii sheria bila shuruti na kwamba, Jeshi la Polisi 
litahakikisha linawachukulia hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

Aidha Sirro amedai kuwa takwimu za uingizwaji na utumiaji wa dawa za kulevya imepungua kwa
 kiasi kikubwa kutokana na kufanyika kwa operesheni za mara kwa mara zinazofanywa na Jeshi hilo 
la polisi.