Magufuli asikitiswa na vifo
Rais John Pombe Magufuli amesikitishwa na vifo vya watu 12 walipoteza maisha katika ajali ya maji baada ya gari aina ya Hiace iliyokuwa imewabeba abiria hao kuteleza kutoka katika kivuko na kuzama kwenye Ziwa Victoria mchana wa leo jijini Mwanza.
Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella na kumtaka kumfikishia salamu zake za pole kwa familia zote zilizopatwa na msiba huo.
“Kwa mshtuko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha baada ya gari la abiria walilokuwa wakisafiria kutumbukia katika ziwa Victoria Mkoani Mwanza, nawapa pole sana wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii, nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ustahimilivu na subira katika kipindi hiki cha majonzi” alisema Rais Magufuli
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi 3 walionusurika katika ajali hii wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Jumla ya watu 12 wamefariki dunia leo mchana kufuatia ajali ya basi la abiria (Daladala) lililozama katika ziwa Victoria baada ya kugonga vizuizi vya kivuko cha Kigongo Wilayani Misungwi na kisha kutumbukia na kuzama majini.
Post a Comment