Wawekezaji wa hivi hatuwataki - Magufuli
Rais Magufuli amefunguka na kusema kuwa Tanzania inahitaji sana wawekezaji kuja kuwekeza nchini lakini wawekezaji ambao wanajifanya kuja kuwekeza kwa kigezo cha kuiba mali za nchi na Watanzania hao hawatakiwi na bora wasije kabisa nchini.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Mererani wakati wa kuzindua barabara ya lami ya kilomita 26 kutoka Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa kilimanjaro (KIA) mkoa wa Kilimanjaro hadi Mererani Manyara Septemba 20, 2017.
Magufuli amesema hayo leo Septemba 20, 2017 akiwa Mkoani Manyara wilaya ya Simanjiro katika ziara yake ya kikazi wakati akizindua barabara na kusema wawekezaji ambao wanataka kuja kuwekeza ili kuiba maliasili za nchi ni bora wasije kwani hawatafanikiwa chini ya utawala wake wa awamu ya tano.
"Tanzania tunahitaji wawekezaji lakini si wawekezaji wanaotaka kutuibia, kama unataka kuja kuwekeza Tanzania kwa kisingizio cha kuja kutuibia ni bora usije, kwani utakuwa umeula wa chuya kwa sababu wakati huu hautaiba, nasema huyo mwekezaji atalia na hili nalisema kwa uwazi kwa sababu tumeamua kupambana kwa ajili ya vita ya uchumi kwa ajili ya taifa letu" alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa mataifa makubwa na wawekezaji kutoka nje wametujengea mawazo kuwa wao ndiyo wenye mali na uwezo kumbe wao hawana hizo mali na uwezo bali sisi ndiyo wenye mali na uwezo huo kuliko wao ambao wanategemea maliasili zetu.
"Tanzania ni tajiri mno, wametujengea 'element' kwamba sisi hatuna wao wanacho, kumbe sisi ndiyo tunacho wao hawana, wengine wanajifanya wafadhili, ndugu zangu viongozi tusimamie rasilimali za nchi yetu nafahamu katika hatua ambazo tumeanza kuchukua wapo baadhi ya watu wameanza kukimbia, wengine hamtawaona wamekimbia kwa sababu wameona walichokuwa wanakifanya ni cha hovyo" alisisitiza Rais Magufuli
Post a Comment